2013-08-14 09:41:50

Kanisa kuu la Utatu Mtakatifu, Ureno kuzinduliwa rasmi hapo tarehe 12 Oktoba 2013


Kardinali Tarcisio Bertone, Katibu mkuu wa Vatican, kuanzia tarehe 12 hadi tarehe 13 Oktoba 2013 anatarajiwa kufanya hija ya kichungaji kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Fatima, nchini Ureno kama sehemu ya Maadhimisho ya Hija ya Kimataifa Madhabahuni hapo.

Uwepo wa Kardinali Bertone unapania kuwa ni alama ya mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro, kama kiini cha ujumbe wa Bikira Maria kwa Watoto wa Fatima, yaani Francis, Yacinta na Lucia.

Itakumbukwa kwamba, kunako Mwezi Oktoba, 2007 katika Maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Miaka 90 tangu Bikira Maria alipowatokea Watoto wa Fatima, Kardinali Bertone, alimwakilisha wakati huo Baba Mtakatifu Benedikto XVI. Wakati huu, Kardinali Bertone anatarajiwa kushiriki katika uzinduzi wa Kanisa kuu la Utatu Mtakatifu, tukio ambalo litafanyika tarehe 12 Oktoba 2013, majira ya jioni kwa saa za Ulaya.

Yote haya yamefafanuliwa kwa kina na mapana na Askofu Antonio Marto wa Jimbo Katoliki la Leiria-Fatima, Ureno, akiwaomba Maaskofu na Waamini nchini Ureno kushiriki kikamilifu katika tukio hli la kiimani hasa wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka wa Imani, uliotangazwa na kuzinduliwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita kama sehemu ya mchakato wa kuimarisha imani katika matendo.







All the contents on this site are copyrighted ©.