2013-08-14 11:51:52

Jamii ishiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya matumizi haramu ya dawa za kulevya!


Rais Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania ameiagiza Wizara ya Afya kupitia kitengo cha magonjwa ya akili pamoja na Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya nchini humo kushirikiana na Kituo cha Ushauri Nasaha cha Pili Misana Foundation, ambacho kinawasaidia waathirika wa dawa ya kulevya ili kiweze kuwahudumia watu wengi zaidi hapa nchini.

Rais Kikwete amesema hayo Ikulu alipokutana na vijana walioachana na matumizi ya dawa za kulevya ambao wamepata ushauri nasaha na usaidizi kutoka katika kituo cha Pili Misana kilichopo Kigamboni jijini Dar es Salaam.“Jamii lazima ishiriki katika utatuzi wa jambo hili, ni tatizo kubwa na linamgusa kila mtu na inabidi wote tushiriki katika kulipiga vita”

Rais amesema na kumpongeza Bi. Pili Misana na Zacharia Hans Pope ambaye ndiye mfadhili wa kituo hicho ambacho tayari vijana wapatao 203 wamepatiwa huduma ya ushauri nasaha na kuweza kuachana na madawa ya kulevya na kurudia katika shughuli zao za kimaendeleo.

Rais Kikwete amesema tatizo la madawa ya kulevya ni la muda mrefu lakini hapo awali lilikuwa halisikiki sana kwa sababu jitihada za kuzuia madawa hayo zilikua hazitangazwi wala kufuatiliwa sana.“Sasa hivi juhudi mbalimbali za kupambana na madawa ya kulevya zinatangazwa na hivyo kusikika sana na pia taarifa nyingi zinazohusiana na madawa ya kulevya zinawekwa wazi kwa jamii” Mhe. Rais amesema na kueleza kuwa taarifa nyingi zinawekwa wazi na kutangazwa ili kushirikisha jamii katika kupambana na tatizo hili.

Kiasi cha vijana 35 wamefika Ikulu ambapo wametoka katika nyanja mbalimbali za kitaaluma, elimu na kijamii na pia umri tofauti kutoka miaka 14 hadi miaka 53. Kituo hicho kinahudumia watu wenye jinsia tofauti wake kwa waume kutoka sehemu mbalimbali nchini.

Rais Kikwete amesema Serikali inafanya jitihada kubwa sana za kuwasaidia vijana mbalimbali na bado itaendelea kutoa msaada huo, huku juhudi mbalimbali za kupambana na madawa hayo zikiendelea.

Naye mfadhili wa kituo hicho Bw. Zacharia Hans Pope ameitaka jamii kushiriki na kuwa karibu zaidi na vijana ili kuweza kusaidia katika mapambano ya madawa ya kulevya na athari zake nchini.








All the contents on this site are copyrighted ©.