2013-08-13 14:43:34

Wanamichezo ni watu wanaobeba utu!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne tarehe 13 Agosti 2013 amekutana na viongozi pamoja na wachezaji wa timu za taifa kutoka Italia na Argentina wanaojiandaa kwa ajili ya kucheza mechi ya kirafiki mjini Roma hapo tarehe 14 Agosti 2013.

Akizungumza na wanamichezo hao, Baba Mtakatifu amekazia kwa namna ya pekee kabisa umuhimu wa kudumisha urafiki katika michezo, kwani kuna umati mkubwa wa watu wanaowafuata wanapokuwa wakitandaza kabumbu uwanjani na hata nje ya viwanja vya michezo.

Hii ni dhamana na wajibu mkubwa kwa wanamichezo. Michezo haina budi kujikita katika: uzuri, majitoleo na urafiki, ikiwa kama mambo haya yanayokosekana uwanjani hapo kuna patashika nguo kuchanika. Katika michezo ubinafsi hauna budi kuwekwa kando ili kujenga moyo na mshikamano wa timu unaosimikwa katika ari, na moyo wa kupenda na kufurahia michezo na wala si kwa sababu ya fedha.

Baba Mtakatifu anasema, wachezaji wa kitaifa na kimataifa hawana budi kujenga na kukuza moyo wa kupenda michezo, jambo ambalo ni jema katika maisha ya kijamii, daima wakitafuta mafao ya wengi yanayojikita zaidi na zaidi katika majitoleo, moyo na uzuri wa michezo.

Wanamichezo wanakumbushwa kwamba, kabla ya kuwa ni watu mashuhuri, wao ni binadamu, wenye karama na mapungufu; mawazo, matumaini na matatizo yao. Hata kama ni mabingwa na watu mashuhuri katika michezo, wanapaswa bado kuendelea kubaki kuwa ni watu katika michezo na maisha. Ni watu wanaobeba utu.

Baba Mtakatifu amewataka viongozi wa michezo kutambua umuhimu wa michezo badala ya kugeuza michezo kuwa ni biashara. Ni wajibu wao kuhakikisha kwamba, watu wanapenda na kufurahia michezo ili hatimaye, kuondokana na tatizo la ubaguzi wa rangi unaojitokeza mara kwa mara kwenye viwanja wa michezo. Wanamichezo wakizingaztia dhamana yao, michezo inakuwa ni fursa ya kuwatajirisha watazamaji na wapenda michezo. Ni mwelekeo unaoweza pia kuondoa uhalifu kwenye michezo na watu kuanza kujisikia kuwa ni watoto wa familia moja.

Baba Mtakatifu Francisko amewakumbusha wanamichezo hao kwamba, alipokuwa kijana mdogo mwenye umri wa miaka kumi hivi, alikuwa anakwenda kuangalia mpira na daima alipokuwa anarudi nyumbani alikuwa ni mtu aliyesheheni furaha. Amewashukuru wanasoka na viongozi wao kutoka Argentina. Amewakumbusha kwamba, wanamichezo ni kioo cha jamii na mfano bora wa kuigwa na vijana wengi kwani wana karama na vipaji vinavyomwilishwa katika maisha.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, ana matumaini na wanamichezo kwa mambo mengi wanayoweza kutenda kwa ajili ya kuwasaidia vijana. Watu wengi wanawaonea wivu, lakini watambue kwamba, wanaweza kuwa ni mfano bora wa kuigwa au wakabezwa na Jamii kutokana na matendo yao. Baba Mtakatifu anawataka wanamichezo kuwa ni mfano wa ukweli na heshima kwa wengine.







All the contents on this site are copyrighted ©.