Onesheni ukomavu wa kisiasa na kidemokrasia kwa kulinda na kudumisha amani na utulivu!
Baraza la Maaskofu Katoliki Zimbabwe linasema linaweza kusaidia upatikanaji wa suluhu
ya amani na upatanisho miongoni mwa vyama vya kisiasa nchini Zimbabwe baada ya Chama
cha upinzani cha MDC kukataa matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika nchini Zimbabwe
hivi karibuni na Rais Robert Mugabe wa Chama cha ZANU-PF akaibuka kidedea kwa kupata
asilimia 62% ya kura halali zilizopigwa na mpinzani wake Morgan Tsvangirai kutoka
Chama cha MDC akapata asilimia 34%.
Baraza la
Maaskofu Katoliki Zimbabwe linawataka wanasiasa kuanzisha mchakato wa majadiliano
ya amani na utulivu kwa ajili ya ustawi na mafao ya wananchi wa Zimbabwe ambao kwa
miaka kadhaa kwa sasa wanateseka kutokana na kinzani za kisiasa nchini humo.
Padre
Frederick Chiromba, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Zimbabwe anasema, viongozi
wa Makanisa nchini humo wanavitaka vyama vya siasa kuonesha uungwana kwa kutafuta
suluhu ya kasoro zilizojitokeza kwenye uchaguzi mkuu kwa njia ya majadiliano, amani
na utulivu.
Wananchi wa Zimbabwe wanahitaji mshikamano wa kidugu na umoja
wa kitaifa ili kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazoendelea kuwakabili. Inasikitisha
kusikia kwamba, nchi nyingi zimeonesha kutoridhishwa na mchakato mzima wa uchaguzi
mkuu nchini Zimbabwe, jambo ambalo linatia kichefuchefu kwa wananchi waliokuwa wana
matumaini ya kuanza upya ujenzi wa nchi yao ambayo inaendelea kupitia hali ngumu ya
maisha na vikwazo kwa kimataifa.
Watazamaji wa kimataifa wameitaka Serikali
ya Zimbabwe kufanya uchunguzi wa kina ili kuweza kubainisha kasoro zilizojitokeza
na kuchukua hatua madhubuti. Chama cha MDC kinachosema kwamba, kimedhulumiwa katika
uchaguzi, kinapaswa kutumia njia halali kufikisha madai yake badala ya kufanya vurugu
kwa maandamano mitaani yanayoweza kuvuruga amani na utulivu nchini Zimbabwe, kiasi
kwamba, watu wakaendelea bado kugawanyika kwa misingi ya kisiasa.
Licha ya
kasoro zinazozungumzwa katika mchakato wa uchaguzi nchini Zimbabwe, lakini jambo la
msingi ambalo viongozi wa Makanisa wanapenda kuwashukuru wananchi wa Zimbabwe ni kufanya
uchaguzi mkuu kwa njia ya amani na utulivu. Inasikitisha kuona kwamba, Zimbabwe bado
inaendelea kutengwa na Jumuiya ya Kimataifa kutokana na kinzani za kisiasa, kwa wanasiasa
kuendelea kutunishiana misuri!