2013-08-13 08:45:23

Jitahidini kuongozwa na mwanga wa imani katika hija ya maisha yenu!


Kardinali Tarcisio Bertone, Katibu mkuu wa Vatican, hivi karibuni, ameushukuru uongozi wa Manispaa ya Introd, katika maeneo ya Les Combes, Kaskazini mwa Italia, kwa kumpatia uraia wa heshima katika mji wao. Kwa kipindi cha miaka minane, Kardinali Bertone, amekuwa akitumia mji huo kwa ajili ya mapumziko ya kipindi cha kiangazi.

Itakumbukwa kwamba, hili pia ni eneo ambalo Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, waliyatumia wakati wa mapumziko ya kipindi cha kiangazi. Lakini eneo hili lina uhusiano wa pekee katika maisha na utume wa Kardinali Bertone, kwani linahudumiwa na Shirika la Wasalesiani wa Don Bosco, chemchemi ya miito na utume wa Kanisa kwa vijana.

Kardinali Bertone anasema, Wasalesiani wanaendelea kufuata nyayo za Mwanzilishi wao kwa kujikita katika majiundo makini kwa vijana wa kizazi kipya, ili kuwarithisha imani, tunu msingi za maisha ya kiutu na kimaadili. Taasisi za Wasalesiani zimeendelea kuwa ni chemchemi ya miito na raia waliofundwa wakafundika kwa ajili ya mafao ya Jamii inayowazunguka. Ni changamoto kwa wanafunzi wanaohitimu kutoka katika taasisi za Wasalesiani wa Don Bosco kuendelea kuwa waaminifu kwa Mungu, Kanisa na Jamii kwa ujumla.

Katika mahubiri yake wakati wa Ibada ya Misa Takatifu amewakumbusha kwamba, Ibada ya Misa takatifu inawaunganisha kwa namna ya ajabu ili kushiriki katika Mafumbo ya Kanisa, ili kuweza kumegeana na kuonjeshana Mapokeo na Utajiri wa amana za Kanisa kama walivyofanya Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI kwa kujenga na kuimarisha urafiki na mshikamano na wananchi wanaoishi katika eneo hili. Historia ya eneo hii itaendelea kukumbukwa na wengi.

Wakati huu ambapo waamini na wananchi wengi Barani Ulaya wako kwenye mapumziko ya Kipindi cha Kiangazi, Kardinali Bertone, anawaalika kwa namna ya pekee kujitajirisha kwa kusoma Waraka wa kichungaji uliotolewa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko, Lumen Fidei, Mwanga wa Imani. Ni waraka ambao umeandaliwa kwa umakini mkubwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto wa kumi na sita na kuboreshwa zaidi na Papa Francisko.

Huu ni mwaliko kwa kila mwamini kuhakikisha kwamba, anaongozwa na Mwanga wa Imani katika hija ya maisha na vipaumbele vyake kwa kumwilisha imani hii katika matendo ya huruma na mapendo kwa jirani, lakini hasa zaidi wale wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Tukio hili limehudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Kanisa na Serikali kutoka katika eneo la Val d' Aosta.







All the contents on this site are copyrighted ©.