Wazee wanang'atuka.. ! Safari ya Waisrael kwenda nchi ya ahadi iliwachukua wana
wa Israeli miaka 40. Musa alipewa kazi hiyo akiwa na umri mkubwa, takribani miaka
80. Yeye anawaambia wana wa Israeli ".. Nina miaka mia na ishirini.." (Kumb 31:2).
Musa anang'atuka na kumuachia kijiti kijana mdogo Joshua. Hii ni sura njema ya wazee
wenye busara na unyoofu wa kuruhusu wakati upeperushe mambo na vitu viende "to let
it go.." Somo la kwanza la Leo Augosti 13, 2013 kutoka kitabu cha Kumbu Kumbu ya
Torati (Kumb 31:1- lataka kutuambia yafuatayo: 1. Ni wajibu kwa wazee kuwaandaa
vijana kwa nafasi mbali mbali za uongozi katika jamii. Na sio tu kuwaandaa - bali
kuwapa moyo, kuwajengea uwezo, kuwaamini na kuwaachia malengo na mikoba. Musa alikabidhiwa
lengo la kuwafikisha wana wa Israeli nchi ya ahadi (kutoka 3:10). Na ndilo lengo la
kudumu analomkabidhi kijana Joshua wakiwa mlima Nebo huku wakikabili bonde la Mto
Yordani. Anamwambia kijana Yoshua, "..jipe moyo, Mungu ndiye atakayepigana vita badala
yenu.." (Kumb 31:7).
2. Kwa wazee ye yote ni vizuri kujikubali kuwa muda wake
umeisha. Kama umekwisha kula chumvi nyingi miaka 60 hadi 75, usipigane vikumbo na
Vijana. Kuna heshima kubwa ya kujiondoa mapema madarakani. Ukijiondoa taratibu na
kwa mpangilio utapata fursa ya kula pensheni yako vizuri na kwa utulivu. Kwa hili
najua ni sawa “kumpigia mbuzi gitaa” tazama wapo wazee wanaoendelea kung’angania madarakani.
3.
Mungu wetu hajafirisika kuwa na viongozi wapya, tena vijana. Mungu wetu ana kina Joshua,
mwana wa Mzee Yese Daudi, Timoteo, Samueli na wengineo. Mungu pia anatumia hata watoto
wadogo. Somo letu la Injili siku ya leo linatupa picha ya Vizee ving'ang'anizi
katika uongozi na madaraka. Wazee hawa hawapendi kuacha upepo wa nyakati, umri na
damu changa uchukue nafasi yake. Wazee hawa huwa wanajiona kuwa wamezaliwa ili kutawala
na hufanya kila liwezekanalo kuhatamia madaraka. Kristu anakemea na kuvunja kabisa
roho hii ya kung'ang'ania madaraka. Anakachukua katoto kadogo na kukaweka kati yao
(Matayo 18:6). Yesu anataka kusema nasi hili katika siku hii : 1. Uongozi ni
wa watu wote. Kuongoza ni kushirikishana na kuonesha dira - yaani, mbinu shirikishi
itumike daima (participatory approach). Katika kushirikisha hata mtoto mdogo, maskini,
mlalahoi, asiyesoma ana kitu cha kuchangia katika Jumuiya yetu kubwa. Maendeleo ni
mchanyato wa mawazo, uzoefu, mang'amuzi na uelewa tofauti wa kila mwana jumuiya.
2.
Tusiwakwaze wadogo na wa tabaka la chini kwa kuona wao kuwa wapo wapo tu. kwamba uwepo
wao katika jumuiya au familia ni kutusindikiza tu sisi wenye majina. Wao nao pia ni
sehemu muhimu ya muhimiri wa maamuzi yetu. Wao si wa kuburuzwa katika maamuzi - "pedagogy
of the oppressed" Wadogo wo wote na wanyonge katika jamii daima huwa na moyo safi,
na daima wanamwona Mungu katika unyonge wao (Matayo 5:8). Hivyo, tuwaogope na kuwaheshimu
maskini na wasio na kitu katika jamii kwa vile wana watetezi muhimu mbinguni, yaani
- malaika.
Tusali kwa ajili ya nchi yetu ya Tanzania ili michakato yote ya
uongozi katika ngazi zote, na hasa ule wa 2015, utawaliwe na roho ya kushirikisha
madaraka - na ikibidi waliokula chumvi nyingi wawe na unyenyekevu wa kama mzee Musa,
wa kung'atuka kutoka madarakani.
Imeandaliwa na Padre Beno Kikudo, Jimbo kuu
la Dar es Salaam.