Familia na changamoto zake katika ulimwengu wa utandawazi, sayansi na teknolojia!
Katika mwaka huu wa imani tunaalikwa kutafakari zaidi na zaidi kuhusu maisha ya familia
kwani uhai wa familia ni uhai wa Kanisa na taifa zima la Mungu. Maisha ya familia
ni zawadi kubwa ambayo Mungu ametujalia tangu pale alipoumba ulimwengu kwani yeye
aliona kuwa “si vema huyu mtu awe peke yake, nitamfanyizia msaidizi wa kufanana naye”
(Mwanzo 2:18). Hapa tunaona hekima
ya Mungu ya kumwumba mume na mke na kuwaambia kuwa “mwanaume atamwacha baba yake na
mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja” (Mwanzo 2:24). Tunaishi
katika ulimwengu wenye changamoto nyingi ambazo tusipokuwa macho zinaweza kuhatarisha
ule umoja kati ya mume na mke, umoja amboa Mwenyezi Mungu anatuambia kuwa “mwanadamu
asiutenganishe” (Mk 10:9). Tunapoendelea kutafakari kuhusu maisha ya familia na
changamoto zake katika ulimwengu wa utandawazi, sayansi na teknolojia, leo hii ningependa
tutafari pamoja kuhusu tatizo la kuvunjika kwa Agano la ndoa kati ya Mume na Mke katika
jamii zetu. Jambo hili linaonekana kama kitu cha kawaida katika ulimwengu wetu wa
leo. Kadiri ya Mafundisho ya Kanisa ambayo msingi wake ni Maandiko Matakatifu
kama tulivyoona, Agano la Ndoa Takatifu ambalo linatambulika na Kanisa kama Sakramenti
linaweza kutenganishwa na Mungu pekee pale kinapotekea kifo cha mwenzi mmoja wapo.
Hivyo basi, pale wenzi wawili(Mume na Mke) wanaposema kuwa wanapendana kwa dhati,
upendo huo sio upendo wa majaribio bali ni upendo unaowaalika wapenzi hao wawili kila
mmoja kujitoa kwa mwenzake mzima mzima bila kujibakisha. Hii hali ya kijotoa kwa
mwingine ni sadaka kubwa katika maisha kwani wapenzi hawa wanakubali kupokeana kama
walivyo katika raha na taabu, maana yake wanakubali kusaidiana kuubeba msalaba wa
maisha katika mazingira yoyote kwa lengo la kuupata utakatifu. Bila shaka kila
mmoja wetu anaweza kuonja madhara makubwa yanayoteka katika jamii pale wenzi wawili
wanapotengana. Kwanza kabisa tunaweza kuonja mahagaiko wanayowapata wenzi hao, lakini
madhara makubwa zaidi tunayouna mateso makubwa wanoyopata watoto kama wenzi hao walijaliwa
zawadi hiyo kutoka kwa Mungu. Katika mazingira hayo, watoto wanashindwa kufurahia
upendo wa Baba na Mama wakati wazazi wao bado wapo hai. Wapendwa, binadamu sio
wasisi wa Agano Takatifu la Ndoa bali ni Mungu peke yake. Mungu anatupatia zawadi
ya maisha ya ndoa na akiwa na lengo la kututaka tutumie vizuri zawadi hiyo kusudi
itusaidie kuupata Utakatifu na mwisho wa maisha yetu hapa duniani tuweze kuwa na muunganiko
mkamilifu naye huko mbinguni. Zawadi hii sio mali yetu na hatuwezi kufanikiwa
kuiihishi kama zilivyo zawadi za miito mngine katika kanisa bila kuwa na ushirikiano
mzuri na yule aliyetupatia zawadi hizo yaani Mungu. Ushirikiano na Mungu unafanyika
katika maisha yetu ya kila siku pale tunapo shiriki kiaminifu katika kutafakari Neno
la Mungu, maisha ya sala na Masakramenti ya Kanisa hasa Sakramenti ya Kitubio na Ekaristi
Takatifu. Leo hii tunaweza kujiuliza sisi wenyewe katika familia zetu; Ni wangapi
kati yetu wana Maandiko Matakatifu nyumbani na ni wangapi angalu tunajitolea muda
Fulani katika siku kumsikiliza Mungu anatueleza nini katika neno lake! Ni wangapi
kati yetu tunafanya sala za familia nyumbani kwetu! Ni wangapi kati yetu tunajipatanisha
na Mungu kwa Sakramenti ya kitubio pale tunapo tenda dhambi na kumpokea Yesu katika
Ekaristi Takatifu! Ndugu zangu wapendwa, tujaribu kujiuliza ni mambo gani katika
ulimwengu wetu wa leo yanayokuwa kikwazo ya kutafuta muda wa kutafari uhusiano wetu
na Mungu? Bila shaka kila mmoja wetu atakuwa na sababu zake. Mwaka huu wa imani tunaalikwa
kutafari tena vikwazo vinayotuweka mbali na Mungu na kujiwekea mikakati ya mabadiliko
ya kweli ya kutoka moyoni. Katika maisha yetu tukumbuke kwamba, hakuna Agano la
ndoa au agano lolote tunaloweka na Mungu linaloweza kusimama imara bila kuwa wanyenyekevu
kwa Mungu na kumweka Mungu kuwa msimamizi mkuuu. Umoja katika maisha ya ndoa unapatikana
pale wanandoa wanapokuwa na mapendo ya kweli kutoka moyoni, mapendo ambayo ni ishara
ya uwepo wa Mungu aliye asili ya mapendo yote katika maisha ya binadamu . Kama Mungu
hana nafasi katika mioyo yetu, kamwe hatuwezi kujua kupenda nini na hali hiyo pia
ni mwanzo wa kuvunjika kwa ndoa zilizo nyingi au kuishi katika migogoro ya kila siku
isiyokuwa na mwisho. Kwa maombezi ya familia Takatifu ya Yesu Maria na Yosefu
tuombe neema ya kutambua thamani ya Agano la ndoa na kuliishi Agano hilo mpaka kufa
na pia Baraka za Mungu katika familia zetu kusudi tuweze kudumu katika imani, matumaini
na mapendo. Amina Kutoka Studio za Redio Vatican ni Mimi Padre Titus Nkane OSB.