2013-08-12 08:13:23

Dhana ya uinjilishaji mpya katika vikosi vya ulinzi na usalama


Baba Mtakatifu Francisko ameridhia ombi la kung’atuka kutoka madarakani lililowasilishwa kwake na Askofu Vincenzo Pelvi, wa Jimbo la kijeshi nchini Italia kutokana na umri. Itakumbukwa kwamba, kunako mwaka 2006 aliteuliwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita kuwa ni Askofu wa Jimbo la Kijeshi nchini Italia. RealAudioMP3

Sr. Gisela Upendo Msuya anatujuza zaidi kuhusu mchango wa Askofu mstaafu Pelvi katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani kwa vikosi vya ulinzi na usalama nchini Italia.

Wanajeshi wa vikosi mbali mbali vya ulinzi na usalama ni watu ambao wanahusishwa mara nyingi na mambo ya vita, vurugu, ulinzi na usalama. Katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, wanajeshi wanachangamotishwa na Mama Kanisa kuchuchumilia wongofu wa ndani na kujikita katika utakatifu wa maisha, huku wakiendelea kutolea ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Hii ndiyo changamoto iliyotolewa hivi karibuni katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani kwa ajili ya wanajeshi nchini Italia, tukio ambalo lilihudhuriwa na walengwa wengi pamoja na viongozi mbali mbali wa Kanisa.

Askofu mkuu Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya uhamasishaji wa Uinjilishaji Mpya amepembua dhana ya Uinjilishaji Mpya katika ulimwengu wa wanajeshi wa vikosi vya ulinzi na usalama. Kwa upande wake, Askofu Vincenzo Palvi wa Jimbo la Majeshi Italia, ameandika na kuchapisha kitabu kinachozungumzia ushuhuda wa imani katika ulimwengu wa wanajeshi wa vikosi vya ulinzi na usalama. Anaweka mbele ya macho yao ya imani viongozi mashuhuri wa Kanisa wanaoweza kuwa ni mfano na kielelezo cha kuigwa katika maisha na utume wao kama wanajeshi.

Baba Mtakatifu Yohane wa Ishirini na tatu, ambaye aliwahi kuwa ni Padre kiongozi wa maisha ya kiroho kwa vikosi vya ulinzi na usalama nchini Italia. Huyu ni mfano bora wa kuigwa katika utakatifu wa maisha. Kuna Mapadre wengi walioonesha ushuhuda wa imani na mwamko wa Uinjilishaji wakati wakitekeleza majukumu yao kwenye Vita kuu ya Pili ya Dunia.

Hawa walikuwa ni sauti ya kinabii, kiasi hata cha kuhatarisha maisha yao, changamoto na mwaliko kwa wanajeshi kuwa waaminifu katika maisha na utume wao ndani ya Jamii na Kanisa katika ujumla wake. Hawa ni viongozi ambao wanaweza kusaidia kuamsha tena dhamiri nyofu katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani.

Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni alisema, ushuhuda wa imani unajidhihirisha katika hali mbali mbali, kumbe hata huduma ya kijeshi inaweza kuwa ni epifania ya utakatifu wa maisha, mahali ambapo, mwamini anafanya hija ya maisha yake ya kiroho, huku akijitahidi kumwilisha ndani mwake, fadhila za maisha ya Kikristo; daima akitafuta mafao ya wengi, utu na heshima ya binadamu; yote haya yawe ni kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mwenyezi Mungu.

Askofu Vincenzo Palvi anasema kwamba, ndani ya Kanisa kuna mifano mingi ya Askari ambao wamekuwa ni watakatifu na mifano angavu ya imani na utu wema. Mama Kanisa anawapongeza na kuwaimbia utenzi wa sifa na shukrani na kwamba, Waraka wa Amani Duniani, Pacem In Terris unaweza kuwa ni mwongozo makini kwa wanajeshi wa vikosi vya ulinzi na usalama.

Maadhimisho ya Mwaka wa Imani kwa viongozi wa kiroho kwenye vikosi vya ulinzi na usalama, yamehudhuriwa na Mapadre 150. Lakini, Askofu mkuu Rino Fisichella anasema, idadi ya walengwa waliohudhuria maadhimisho hayo si mali kitu, jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, kila mwanajeshi anatekeleza wajibu wake barabara; Mapadre waoneshe ushuhuda wa maisha yao ya Kipadre.

Uinjilishaji Mpya ni mchakato ambao unapaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha yakila siku, kwa kutambua kwamba, kila mwamini anachangamotishwa kuwa ni mhudumu wa furaha ya Injili inayobubujika kutoka kwa Kristo mwenyewe. Waamini wajibidishe kumfahamu Kristo na Injili yake na kutambua kwamba, Jumuiya ya Kikristo inatumwa kutangaza na kushuhudia kweli za Kiinjili.

Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, waamini wanatolea ushuhuda wao imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, kwani maneno matupu kamwe hayawezi kuvunja mfupa!








All the contents on this site are copyrighted ©.