Balozi wa Vatican nchini Kenya aanza utume wake rasmi!
Askofu mkuu Charle s Daniel Balvo, Balozi wa Vatican nchini Kenya na Mwakilishi wa
kudumu wa Vatican kwenye Shirika la umoja wa Mataifa linaloshughulikia mazingira,
UNEP na Shirika la Makazi ya Watu la Umoja wa Mataifa, UN habitat, ameanza utume wake
kwa makaribisho makubwa yaliyoongozwa na Kardinali John Njue, Rais wa Baraza la Maaskofu
Katoliki Kenya kwa niaba ya Familia ya Mungu nchini Kenya.
Akizungumza na
waandishi wa habari katika tukio hili, Askofu mkuu Balvo amesema kwamba, Baba Mtakatifu
Francisko amemtia ari na moyo wa kutekeleza wajibu na dhamana yake mpya, kwa kutambua
kwamba, anaendelea kumsindikiza kwa njia ya sala na uwepo wake wa karibu. Amepata
nafasi pia ya kukutana na kuzungumza na viongozi wa Kanisa Katoliki nchini Kenya
pamoja na wawakilishi wa Taasisi mbali mbali za Kanisa zenye makao makuu yake nchini
Kenya.
Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Balvo aliwasilisha hati zake za utambulisho
kwa Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, hapo tarehe 28 Juni 2013. Rais Kenyatta alimhakikishia
Askofu mkuu Balvo ushirikiano mkubwa kutoka katika Serikali na kwamba ni msaada mkubwa
kwa Kanisa na Kenya katika ujumla wake. Askofu Balvo amewasilisha pia hati zake kwenye
Mashirika ya Umoja wa Mataifa yenye makao yake makuu Jijini Nairobi.
Baraza
la Maaskofu Katoliki Kenya limemwalika rasmi Askofu mkuu Charles Daniel Balvo kushiriki
katika mkutano wao mkuu unaotarajiwa kufanyika Jimbo kuu la Mombasa na huo ndio utakaokuwa
muda muafaka wa kuwasilisha hati zake za utambulisho kutoka kwa Kardinali Tarcisio
Bertone, Katibu mkuu wa Vatican.