Balozi wa Vatican nchini Benin aanza utume wake rasmi!
Askofu mkuu Brian Udaigwe, Balozi wa Vatican nchini Benin, hivi karibuni ameanza utume
wake nchini Benin kwa kuwasilisha hati za utambulisho kwa Serikali ya Benin. Katika
tukio hili, Askofu mkuu Udaigwe alipata fursa ya kubadilishana mawazo na viongozi
wakuu wa Benin kuhusu hija ya kichungaji iliyofanywa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto
wa kumi na sita, wakati wa kuwasilisha matunda ya Maadhimisho ya Awamu ya Pili ya
Sinodi ya Maaskofu wa Afrika.
Viongozi hao wameguswa kwa namna ya pekee na
kipaumbele kinachoendelea kutolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa maskini na utunzaji
bora wa mazingira. Askofu mkuu Udaigwe aliwasilisha salam na matashi mema kutoka kwa
Baba Mtakatifu Francisko kwa Rais Thomas Boni Yayi wa Benin. Serikali inalishukuru
Kanisa Katoliki katika mikakati inayopania kumwendeleza mtu mzima: kiroho na kimwili
na kwa ajili ya mafao ya wananchi wa Benin katika ujumla wao.
Rais Thomas Boni
Yayi anasema amekuwa ni Rais wa kwanza kutoka Afrika kuweza kukutana na kuzungumza
na Baba Mtakatifu Francisko mara tu baada ya kuchaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki.
Kwa pamoja viongozi hawa wawili wameendelea kuhimiza umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa
kushirikiana katika mchakato wa kudumisha misingi ya haki, amani, utulivu, maendeleo
na mafao ya wengi.
Hivi karibuni Askofu mkuu Brian Udaigwe amepata fursa ya
kukutana na kuzungumza na viongozi mbali mbali wa Kanisa na Kijamii nchini Benin pamoja
na kuwasilisha hati za utambulisho kwa viongozi wa Kanisa kutoka kwa Kardinali Tarcisio
Bertone, katibu mkuu wa Vatican.
Amepongeza ushuhuda na mwamko wa kimissionari
uliooneshwa na Familia ya Mungu nchini Benin pamoja na wale waliofika nchini Benin
kwa ajili ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu. Wakavumilia taabu na mahangaiko mengi,
lakini matunda ya utume wao yanaendelea kuchanua katika medani mbali mbali za maisha
nchini Benin.