Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 19 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa
Tunakutana tena mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican katika kipindi tushirikishane
Neno la Mungu kila Dominika. Ni Dominika ya 19 ya mwaka C.
Mwaliko ni
subira wakati tukitenda kazi kwa ukarimu na kwa furaha mpaka atakapokuja Bwana wa
mavuno Bwana katika Injili anatufundisha kuwa tayari tukizitenda kazi zetu vema yaani
tukitimiza mapenzi ya Mungu. Tunaalikwa daima kuwa watu wa kesha. Neno kesha haliondoi
wajibu bali linatualika kubaki macho tukitenda jambo mwafaka kadiri ya mapenzi ya
Mungu.
Mpendwa msikilizaji kumsubiria Bwana kwaweza kupelekea katika mawazo
ya kutofanya kazi kama yalivyokuwa mawazo katika karne za kwanza za Kanisa, mawazo
ambayo tunayapata hata katika Waraka wa Pili wa Mtakatifu Paulo kwa Watesalonike.
Mara moja Paulo alikemea jambo hilo na kuwaonya wafanye kazi kwa ajili ya mkate wao
wa kila siku. Ndiyo kusema hivi leo lazima kujibidiisha katika kuufanya ulimwengu
uwe mahali pazuri pa kuishi na mahali ambapo utukufu wa Mungu unajidhihirisha wazi.
Katika kuwajibika katika ulimwengu huu lazima kuyatazama yaliyo ya juu yaani
kutafuta kuokoa roho zetu. Katika kutawala ulimwengu huu Injili inatudai kuongoza
vema mali ya mwenye mali, yaani mali na utajiri tuliokabidhiwa. Injili haidai faida
bali inadai kutumia vema mali kwa ajili ya wale waliokuwa wategemezi wake!
Mpendwa
mwana wa Mungu, tunapaswa kuiga mfano wa Mitume wakati wa mwujiza wa mikate jinsi
ambavyo walijibidiisha kugawa chakula kwa walengwa wa Bwana. Huu ndio wajibu wa Kanisa
kuhakikisha kila mmoja aliyemwana wa Mungu anapata habari njema itokayo katika Neno
la Mungu. Neno la Mungu ndio mkate wa uzima na kwalo watu wapate uzima wa milele.
Vivyo hivyo wazazi wanawajibika katika familia zao kutoa mkate wa kila siku katika
nyanza zote mbili, kiroho na kimwili.
Mpendwa msikilizaji katika kutenda kazi
ya Bwana tunapaswa pia kuzingatia moyo wa huduma na si hicho tunachokifanya, hapa
ndo kuna Roho ya Injili ya Bwana. Tunasubiria ujio wa pili wakati tukijenga roho ya
huduma na mapendo kwa wengine. Huo ndio utajiri wa kweli.
Mpendwa kuna jambo
jingine muhimu ambalo yatupasa kulitafakari katika kusubiria na kutenda kazi zetu
yafaa kupambanua wapi tunaweka moyo wetu. Daima Injili inasema kama mmoja akiweka
akiba yake benki basi moyo wake waweza kulala pale na mwingine akiwekeza katika majengo
na ardhi basi moyo huelekea huko! Basi Bwana atuonya kuchagua mahali ambapo roho yetu
ikilala huko basi inahakika ya wokovu. Kusubiri kwetu lazima kukae katika kujenga
furaha ya kimungu furaha itakayotupatia nafasi ya uzima wa milele.
Hatua nyingine
ambayo tunapaswa kuitafakari ni hatua ya kifo. Injili haisemi juu ya kifo bali inazungumza
juu ya Ujio wa Bwana. Kifo hatujui siku wala saa vivyo hivyo hatujui ujio wa Bwana
ni lini! La msingi ni kujiandaa kwa ajili ya yote mawili. Kifo ni mlango wa kumwelekea
Bwana, kama tutajiandaa na hivi tutaweza mapema kukabiliana na woga na hofu itujiayo
mara tusikiapo kifo.
Tujiulize swali sasa kama Bwana angekuja sasa tungewasilisha
nini mbele yake? Kaza moyo mwana wa Mungu katika kuhudumu taifa lake ambayo ndiyo
zawadi yako kwake. Hata hivyo Bwana ni mwenye huruma atafunika mipasuko yetu, cha
msingi tuishi maisha ya huduma kwa wengine. Tumsifu Yesu Kristo.
Tafakari hii
imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya, C.PP.S.