Msamaha ni hatua muhimu katika mchakato wa upatanisho wa kweli!
Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani, Ijumaa tarehe
9 Agosti 2013 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, ikishirikiana na Baraza la Maaskofu
Katoliki Japan, kama sehemu ya kumbu kumbu ya wahanga wa Vita kuu ya Pili ya Dunia.
Japan inakumbuka tarehe 9 Agosti 1945 mji wa Nagasaki ulipolipuliwa kwa bomu
la atomic na hivyo kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Kardinali Turkson
anasema kwamba, msamaha ni hatua muhimu sana katika mchakato wa kujipataanisha na
hatimaye kudumisha amani ambayo kimsingi ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayomwajibisha
mwanadamu.
Mwanadamu akishirikiana kwa ukamilifu na mpango wa Mungu, amani
ya kudumu na endelevu inaweza kutawala katika mioyo ya watu. Kumbe, kuna haja kwa
kila mtu kisimama kidete kulinda na kutetea misingi ya haki, amani na upendo, ili
watu waonje pia huruma ya Mungu.
Kardinali Turkson anasema, kwa njia ya Yesu
Kristo Mwenyezi Mungu ameweza kujipatanisha na wanadamu, mwaliko kwa waamini kutubu
na kumwongokea Mungu, huku wakionesha moyo wa unyenyekevu na kwamba, Mwenyezi Mungu
ndiye anayeweza kumkirimia mwanadamu furaha na amani ya ndani kama Kristo mwenyewe
anavyofafanua katika Heri nane za Mlimani.
Utajiri na umaarufu wa mtu ni mambo
ya mpito kamwe hayawezi kuzima kiu na njaa inayobubujika kutoka katika undani wa mtu.
Yesu mwenyewe amewafundisha wafuasi wake kwa kusema kwamba, amani ya kweli ni zawadi
kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kila mwamini ajibidishe kutafuta amani kwa njia ya sala
na ushuhuda wa maisha yake kama mfuasi amini wa Kristo.
Kwa Ibada ya Misa
Takatifu na Baraza la Maaskofu Katoliki Japani, Kardinali Peter Turkson amehitimisha
ziara yake ya kikazi nchini Japan kama sehemu ya Maadhimisho ya Miaka 68 tangu Japan
iliposhambuliwa kwa mabomu ya Atomic na kusababisha maafa makubwa katika miji ya Hiroshima
na Nagasaki.