Vijana msijifanye kuwa "bize" kiasi hata cha kukosa muda wa majitoleo kwa wale wanaowazunguka!
Noma hiyo!
Queen Said Mratibu wa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio nchini Tanzania katika mahojiano
na radio Vatican anasema kwamba, alipokuwa chuoni alijiunga na Jumuiya ya Mtakatifu
Egidio baada ya kuguswa na moyo wa huduma na majitoleo yaliyokuwa yanafanywa na wanachama
hao.
Anasema, kwa
njia ya Jumuiya, kijana anaweza kugundua shida na mahangaiko ya watu wanaomzunguka,
akaguswa na kubadilishwa mintarafu mwanga wa Injili.
Anasema, falsafa inayoongoza
maisha yake ni kujitosa kimasomaso kwa ajili ya wengine, hasa wale wanaosukumizwa
pembezoni mwa jamii na kwa njia hii ameonja neema na baraka tele katika hija ya maisha
yake ya ujana. Anasema, kuna faida kubwa kwa kijana anapojitoa kwa ajili ya kuwahudumia
wengine na kwamba, muda ni zawadi ambayo kila kijana amebarikiwa kuwa nayo, jambo
la msingi ni kuangalia jinsi ambavyo kijana anavyoutumia muda wake. Vijana wanadhani
kwamba, wako "Bize" kiasi cha kukosa muda kwa ajili ya jirani zao, jambo hili si kweli!
Queen
Said anasema kwamba, kundi la waamini walei na hasa vijana ni kubwa sana ndani ya
Kanisa, ikilinganishwa na Makleri au watawa, kumbe waamini walei wanahamasishwa kushiriki
kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa, kwa njia ya ushuhuda wa imani yao kwa
Kristo na Kanisa lake, ili kuyatakatifuza malimwengu. Kwa namna ya pekee kabisa, vijana
waoneshe ile furaha ya kuwa ni mfuasi wa Kristo.
Vijana wajitahidi kufanya
kazi halali na waendelee kufungua akili na miyo yao ili kuguswa na shida pamoja na
mahangaiko ya watu wanaowazunguka kama anavyoendelea kukazia Baba Mtakatifu Francisko.
Queen Said anasema, Baba Mtakatifu anawapenda na kuwathamini vijana, anawatuma kuwa
ni mashahidi na wadau wa Uinjilishaji Mpya kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao. Ni
changamoto kwa vijana kuachana na uvivu na tabia ya kupenda kubweteka!
Anatumia
fursa hii pia kuwakaribisha vijana wanaojisikia kuguswa na shida pamoja na mahangaiko
ya jirani zao, kujiunga na Jumuiya ya Mtakatifu Egidio ambayo inatekeleza utume wake
katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.