2013-08-08 12:04:11

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaipongeza Kenya kwa kudumisha demokrasia, amani na utulivu!


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amezipongeza juhudi zilizochukuliwa na Jamhuri ya Kenya katika kujiletea maendeleo ikiwa ni pamoja na kuitumia vyema demokrasia kwa kufanya uchaguzi kwa njia ya amani na utulivu. Dk. Shein aliyasema hayo wakati alipokuwa na mazungumzo na Balozi wa Kenya nchini Tanzania Mhe. Mutinda Mutiso aliyefika Ikulu mjini Zanzibar kwa ajili ya kuaga baada ya kumaliza muda wake wa kazi nchini Tanzania.

Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa mafanikio yaliopatikana kutokana na kufanya uchaguzi wa kihistoria nchini humo uliofanyika mwezi Machi mwaka huu, yameweza kuijenga sifa kubwa Kenya ndani na nje ya bara la Afrika. Alieleza kuwa Zanzibar inathamini sana uhusiano na ushirikiano wa kidugu na wenye historia uliopo kati ya Kenya na Zanzibar hasa ikizingatiwa kuwa nchi zote zipo katika Mwambao wa Afrika Mashariki.

Pamoja na hayo, Dk. Shein alipongeza juhudi binafsi alizozichukua Balozi huyo kwa kutunga kitabu kinachoelezea ‘Istilahi za Kidiplomasia’ alichokiandika kwa lugha ya Kishwahili. Dk. Shein alimsifu Balozi huyo kwa jitihada zake binafsi za kuhakikisha kuwa mbali ya kufanya kazi zake za ubalozi wakati hapa nchini pia, ameweza kutunga kitabu hicho ambacho kitamjengea ukumbusho mkubwa katika maisha yake.

Naye Balozi Mutiso alimueleza Dk. Shein kuwa ameweza kupata mafanikio makubwa sana katika utendaji wake wa kazi hapa Tanzania na kusisitiza kuwa nchi yake itaimarisha uhusiano na ushirikiano na Tanzania ikiwemo Zanzibar. Alieleza kuwa nchi yake imo katika juhudi za kuhakikisha inaimarisha uhusiano na ushirikiano huo kati yake na Tanzania kwa kukuza mashirikiano ya kisekta ikiwemo sekta ya nishati ambapo hivi karibuni viongozi wa nchi hiyo walikuja Tanzania kwa lengo hilo.

Alisisitiza kuwa kuwepo kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki kumeweza kupanua zaidi ushirikiano miongoni mwa nchi mbili hizo. Aidha, Balozi Mutiso alimueleza Dk. Shein mafanikio yaliopatika nchini Kenya yakiwemo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa hali ambayo imeipelekea nchi hiyo kuweza kufanya uchaguzi wake kwa amani na utuli mkubwa.

Sanjari na hayo, Balozi huyo alieleza kuwa umefika wakati kwa nchi zilizomo katika bara la Afrika kutatua matatizo yake wenyewe kutokana na mafanikio inayoendelea kuyapata katika sekta mbali mbali. Balozi Mutiso, alieleza kuwa katika kipindi chake cha kazi nchini ameweza kutunga kitabu kinachojulikana kwa jina la ‘Istilahi za Kidiplomasia’ambacho amekikamilisha baada ya kupata miongozo kutoka Taasisi mbali mbali ikiwemo Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni ya Zanzibar. Aidha, alieleza juhudi zinazochukuliwa na Kenya katika kuimarisha lugha ya Kiswahili hivi sasa.

Wakati huo huo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alifanya mazungumzo na Balozi Mdogo wa Oman Mhe. Saleh Suleiman Al-Harith, aliyekuja kujitambulisha kwa Rais. Katika mazungumzo hayo yaliofanyika Ikulu mjini Zanzibar viongozi hao walizumgumza masuala mbali mbali yaliyojikita katika kukuza na kuimarisha uhusiano wa kihistoria uliopo kati ya nchi mbili hizo.

Dk. Shein alimkaribisha nchini Balozi huyo na kumuahidi kuwa Zanzibar itaendeleza uhusiano na ushirikiano uliopo na kumueleza jinsi inavyothamini juhudi za nchi hiyo za kuiunga mkono katika kuimarisha sekta za maendeleo ukiwemo uendelezaji wa baadhi ya majengo katika Chuo cha Afya kili Mbweni. Naye Balozi Saleh Al-Harith alimuhakikishia Dk. Shein kuwa Oman itaendeleza uhusiano na ushirikiiano wake wa kidugu kati yake na Zanzibar.








All the contents on this site are copyrighted ©.