2013-08-08 09:10:54

Kheri na baraka katika Maadhimisho ya Siku kuu ya Id El Fitri


Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa waamini wa dini ya Kiislam, kilikuwa ni kipindi cha kufunga, kusali na kutoa sadaka. Baba Mtakatifu Francisko kwa mara ya kwanza amewaandikia waamini wa dini ya Kiislam salam na matashi mema wanapoadhimisha Siku kuu ya Id El Fitri. Kauli mbiu ya salam hizi ni kuhamasisha hali ya kuheshimiana kwa njia ya elimu.

Kardinali Jean Louis Tauran, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini anasema, ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa waamini wa dini ya Kiislam wakati huu wanapoadhimisha Siku kuu ya Id El Fitri unaonesha jinsi ambavyo anaendelea kutoa kipaumbele cha pekee katika kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na waamini wa dini ya Kiislam, kama alivyokuwa anafanya wakati wa maisha na utume wake nchini Argentina.

Anasema, waamini wa dini hizi mbili wanapaswa kujenga na kuimarisha utamaduni wa kuheshimiana na kuthaminiana katika masuala ya: Imani na Nyumba za Ibada, dhamana ambayo inapaswa kutekelezwa zaidi na viongozi wa dini zote mbili kwa kutoa majiundo makini kuhusu imani zao.

Kanisa Katoliki bado linaendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini bila ya kukata tamaa hata kama matokeo yake bado hayajaridhisha sana. Waamini wa dini hizi mbili watambuane kwamba, wako katika hija ya kumtafuta Mwenyezi Mungu mintarafu imani zao na wala kamwe si maadui wanaosigana mara kwa mara hata katika mambo ya kawaida.

Serikali na wananchi wa Ulaya wanapaswa kujielimisha zaidi kuhusu Uislam na dini ya Kiislam; kupambanua kwa kina na mapana tofauti kati ya imani na waamini wenye misimamo mikali ya kiimani. Kila mtu anao uhuru wa kuabudu na kushuhudia imani yake, kwa kuheshimu na kuthamini pia dini za wengine. Uelewa huu wa kina anasema Kardinali Tauran ni jitihada ambazo zinapaswa kufanyika kuanzia katika familia, shule na kwenye taasisi za elimu ya juu.

Waamini wa dini mbali mbali wajenge utamaduni wa kuheshimiana na kuthaminiana; kupendana na kusaidiana daima wakikuza urafiki unaopania kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini, ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Bila urafiki wa dhati, hakuna uwezekano wa kufanya majadiliano ya kweli!

Kardinali Tauran anasema, Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, amekuwa na mchango mkubwa katika mchakato wa majadiliano ya kidini na waamini wa dini ya Kiislam katika utume wake. Amebahatika kutembelea Misikiti mikubwa mitatu. Hii ndiyo njia na hamu ya Papa Francisko anayotaka kuendeleza katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, ili waamini wa dini hizi mbili waweze kufahamiana, kuheshimiana na kupendana zaidi.

Baba Mtakatifu tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki, amebahatika kukutana na viongozi mbali mbali wa dini ya Kiislam. Amewaonesha moyo wa upendo na ukarimu, anatambua matatizo na changamoto zilizoko mbele yao, kwa pamoja wanaweza kushikamana na kusonga mbele kwa imani na matumaini . Kuna baadhi ya nchi ambazo waamini wa dini ya Kiislam wanabaguliwa kwa misingi ya imani, kama ilivyo pia hata kwa Wakristo katika baadhi ya nchi.

Ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, urafiki na upendo kati ya waamini wa dini ya Kiislam na Kikristo, kuna haja kwa vyombo vya habari kuwa makini katika kuhabarisha, lakini kabla ya kuhabarisha, inawabidi wajifunze zaidi ili kile watakachosema na kuandika, kiwe ni kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Watu waondokane na ujinga wa kutofahamu mambo, hali ambayo wakati mwingine inasababisha kinzani na migogoro ya kidini na kitamaduni.

Kardinali Jean Louis Tauran, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini anahitimisha mahojiano na Radio Vatican kwa kusema kwamba, kuna haja ya kutoa kipaumbele cha kwanza katika mambo mema na mazuri yanayowaunganisha watu katika mshikamano wa upendo badala ya kuendelea kukazia mambo ya misimamo mikali ya kidini, ingawa ni jambo ambalo ni la hatari katika maisha, ustawi na maendeleo ya nchi yoyote ile.







All the contents on this site are copyrighted ©.