2013-08-08 11:47:22

Epukeni utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu; simameni kidete kujenga amani ya kweli inayobubujika kutoka moyoni!


Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani, Alhamisi tarehe 8 Agosti, 2013 ameshiriki katika Ibada ya Sala kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea wahanga wa Vita kuu ya Pili ya Dunia, lakini kwa namna ya pekee, wale waliofariki dunia hapo tarehe 9 Agosti 1945 kwa bomu la atomic lililorushwa mjini Nagasaki. Ibada hii imefanyika kwenye Uwanja maarufu "Ground Zero Park".

Katika Ibada hii, Kardinali Turkson amewakumbuka na kuwaombea binadamu wote wanaoendelea kuteseka katika vita, njaa na magonjwa; amewakumbuka wahamiaji na wakimbizi; wahanga wa maafa na majanga asilia pamoja na wale wote wanaonyanyasika na kudhulumiwa, katika ulimwengu wa utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu wengine. Hii ndiyo changamoto iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati alipotembelea Kisiwa cha Lampedusa.

Kardinali Turkson ameendelea kusali pia kwa ajili ya wananchi wa Japan wanaoendelea kuathirika kutokana na mionzi ya Nyuklia, mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kujenga utamaduni wa haki na amani, ili Jamii ziondokane na wasi wasi wa mashambulizi ya silaha za kinyuklia. Ni matumaini yake kwamba, waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wataendelea kutembea katika mwanga wa upendo wa Mungu, ili kuondokana na vitendo vya uvunjaji wa misingi ya haki na amani na kamwe watu wasiendelee kuomboleza kutokana na vita.

Kardinali Turkson anamwomba Bikira Maria Malkia wa Amani nchini Japan kuwasaidia waamini kutambua kwamba, amani ya kwanza wanayopaswa kuitafuta ni kuondoa dhambi kutoka mioyoni mwao; ili wakiwa safi na huku wamejipatanisha na Mungu pamoja na jirani waweze kuwa kweli ni vyombo vya ujenzi wa amani, wakitoa fursa pia kwa Roho Mtakatifu kutekeleza kazi yake kama sehemu ya mchakato wa mwendelezo wa kazi ya Ukombozi iliyoanzishwa na Yesu Kristo mwenyewe, Bwana na Mfalme wa Amani.







All the contents on this site are copyrighted ©.