2013-08-07 08:20:16

Utamu wa imani shirikishi inayojionesha miongoni mwa vijana! Yaani, we...!


Kardinali Oscar Andrès Rodriguez Maradiaga, Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis anasema, Maadhimisho ya Siku za Vijana Duniani ni nyenzo kubwa katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. RealAudioMP3

Kwa mwaka huu, vijana na watu wenye mapenzi mema, wameonja uzuri wa zawadi ya imani shirikishi, vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia, walipokusanyika mjini Rio de Janeiro, Brazil kusherehekea zawadi ya imani na Baba Mtakatifu Francisko.

Brazil imeonesha chemchemi ya matumaini mapya kutoka Amerika ya Kusini. Matukio ambayo yamewaacha vijana wengi wakiwa wamepigwa na butwaa katika hija ya maisha yao ya imani ni katika Kesha la kufunga Maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013.

Vijana walijiandaa kikamilifu kwa tukio hili kwa kujitakatifuza katika Sakramenti ya Upatanisho, wakamfuata Yesu kwa tafakari ya kina wakati wa Njia ya Msalaba iliyojaa utajiri mkubwa wa changamoto zinazowakabili vijana katika maisha yao hapa duniani, mwishoni, vijana wengi waliweza kushiriki Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Licha ya umati mkubwa wa vijana kwenye Ufuko wa Copacabana, lakini walionesha ibada na uchaji mkuu wakati wa kuabudu Sakramenti ya Ekaristi Takatifu.

Bado vijana wengi wanalikumbuka tukio kama hili wakati wa Maadhimisho ya Siku ya 27 ya Vijana Duniani kwa mwaka 2011 iliyofanyika Jimbo kuu la Madrid, Hispania, Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita alipoamua kubaki na bahari ya vijana iliyokuwa inanyeeshewa na mvua, kiasi kwamba, hata yale mahubiri yake yakalowa chapachapa kwa matone ya mvua! Huu ni ushuhuda wa imani kwa Yesu wa Ekaristi Takatifu, mkate wa uzima, ulioshuka kutoka mbinguni, chakula cha wasafiri.

Kardinali Maradiaga anaendelea kusema kwamba, Makongamano ya Ekaristi Takatifu katika ngazi ya Parokia, Kijimbo, Kitaifa au Kimataifa yamekuwa na mvuto mkubwa katika maisha ya waamini wengi. Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu kwenye ufuko wa Copacabana, ilikuwa na mvuto wa pekee, kutokana na uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko ambaye anaendelea kuwa ni kipenzi cha wengi.

Maadhimisho ya Siku za Vijana ni nyenzo inayowasaidia vijana na waamini kwa ujumla kugundua furaha ya imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Ni chemchemi ya miito mbali mbali ndani ya Kanisa na mwaliko kwa vijana kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano miongoni mwao na Kanisa katika ujumla wake. Waamini walioshiriki kwa namna moja au nyingine tangu kuanzishwa kwa Maadhimisho haya na Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili, wameendelea kuwa ni msaada mkubwa kwa maisha na utume wa Kanisa.

Kardinali Maradiaga anasema, hata wale ambao imani yao ilikuwa inaanza kuota ukutu na ukakasi wa maisha ya kiroho, wameweza kupata tena cheche za matumaini ya kuanza upya na hija ya maisha yao ya kiroho! Huu ndio utamu wa imani shirikishi inayojionesha kwa namna ya pekee miongoni mwa vijana.

Kila mahali ambapo Maadhimisho haya yamefanyika, hapo waamini na watu wenye mapenzi mema wameshuhudia neema na baraka za Mungu kwa ajili ya watu wake. Hizi ni nyakati zinazoleta ari na mwamko mpya katika imani, matumaini na mapendo, fadhila za Kimungu. Waamini kwa namna ya ajabu wanapata mvuto na mguso wa cheche za Injili wanapokutana na vijana wakitembea makundi kwa makundi katika miji yao si haba.

Kardinali Oscar Maradiaga anasema, kwa mwaka huu, Rio wengi wanasema imefunika! Hii inatokana na ukweli kwamba, Baba Mtakatifu Francisko alijimwaga miongoni mwa wananchi wa Brazil bila ya hofu wala mashaka. Akawa tayari kuwanyooshea mikono wote waliotaka kumsalimia! Hakuwa na wasi wasi wa kupokea na kunywa kile watu ambacho walimpatia kwa moyo wa upendo na ukarimu! Haya ni matendo yanayobakiza chapa katika maisha ya watu!

Ni maneno, matendo na ushuhuda unaowaachia watu wengi matumaini mapya katika maisha yao. Kanisa linaendelea kumshukuru Mungu kwa uwepo wa Papa Francisko ambaye anaendelea kulipyaisha Kanisa na kulifanya kuishi kipindi cha neema, mwaliko kwa kila mwamini kutekeleza wajibu wa kumshuhudia Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka wafu kwa maneno na matendo adili!

Imehaririwa na Padre Richard Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.