2013-08-07 08:34:35

SECAM katika mchakato wa kumwilisha misingi ya haki, amani na upatanisho Barani Afrika


Hali ya Bara la Afrika; Uinjilishaji wa kina; Toba na Wongofu wa ndani; Majadiliano ya kidini na kiekukeme pamoja na maazimio ni kati ya mambo makuu yaliyojadiliwa na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar. RealAudioMP3
SECAM katika mkutano wake wa kumi na sita, uliohitimishwa hivi karibuni huko Kinshasa, DRC. Wajumbe wa SECAM wameamua kuadhimisha Mwaka wa Upatanisho Barani Afrika, kama njia ya kuenzi mchango mkubwa uliotolewa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita baada ya kuchapisha Waraka wake wa kichungaji, Africae Munus, Dhamana ya Afrika, hapo mwaka 2011.

Maadhimisho ya Mkutano mkuu wa SECAM kwa mwaka huu yameongozwa na kauli mbiu “ Kanisa, familia ya Mungu Barani Afrika katika huduma ya haki, amani na upatanisho. SECAM imetoa Maazimio ambayo yanapaswa kutendewa kazi na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, kwa kutambua kwamba, kama Kanisa, linapaswa kuwa mstari wa mbele kupambana fika na ubaguzi, nyanyaso na mifumo yote ile ambayo inadhalilisha utu na heshima ya binadamu, kwa kujisafisha kutoka katika undani wa Kanisa lenyewe.

Kanisa halina budi kusimama kidete kuzungumza ukweli na uwazi kama sehemu ya mchakato wa kupambana na sera za kisiasa, kijamii na kidini kwa kuonesha nafasi ya Kanisa kama familia ya Mungu katika huduma ya haki, amani na upatanisho.

SECAM imejiwekea mikakati madhubuti ya kushirikiana na Vyuo vikuu pamoja na taasisi za elimu ya juu zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki Barani Afrika katika kukoleza na kuimarisha majiundo ya mtu mzima: kiroho na kimwili: kwa kukazia Mafundisho Jamii ya Kanisa, hasa miongoni mwa waamini walei, ili waweze kushiriki katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao.

SECAM imewataka waamini wa Kanisa Katoliki Barani Afrika na watu wenye mapenzi mema, kutambua, kuheshimu na kuendeleza dhamana, utu na heshima ya ndoa ya Kikristo na Familia kadiri ya mpango wa Mungu kwa maisha ya mwanadamu na kadiri ya tunu msingi za Kiinjili. Wajumbe wa SECAM wanatambua na kuthamini mchango wa wanawake katika mikakati ya upatanisho, haki, amani na Uinjilishaji wa kina; wanawake wapewe fursa ili waweze kuchangia karama na utajiri wao katika maisha na utume wa Kanisa.

SECAM inawataka kwa namna ya pekee viongozi Wakatoliki kutoelemewa na uchu wa mali na madaraka, bali watambue kwamba, uongozi ni kwa ajili ya huduma kwa jirani zao na wala si fursa ya kujilimbikizia mali. Watumie karama, taaluma na mafanikio walio bahatika kupata kama baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kudumisha na kuendeleza misingi ya haki, amani na upatanisho wa kweli; daima wakiwa mstari wa mbele kulinda na kutunza mazingira, kazi ya uumbaji ambayo mwanadamu amekabidhiwa na Mwenyezi Mungu.

SECAM ina shauri kwamba, kila Jimbo Barani Afrika liunde Tume ya Haki na Amani pamoja na kuibua mbinu mkakati utakaoliwezesha Kanisa Barani Afrika, kuweza kumwilisha ujumbe wa Dhamana ya Afrika katika maisha na vipaumbele vyake! SECAM pia inatambua umuhimu wa majadiliano ya kidini na kiekumene miongoni mwa waamini na wananchi wanaoishi Barani Afrika.

Majadiliano ni nyenzo muhimu kwa ajili ya kudumisha msingi wa haki, amani na upatanisho Barani Afrika, changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutolea ushuhuda wao kama nyenzo ya kushirikishana upendo wa Mungu kwa watu wote.

SECAM inasema, majadiliano haya hayana budi kujikita katika ukweli, heshima na uvumilivu sanjari na kuwa na mikakati kwa ajili ya maendeleo endelevu kwa ajili ya mafao ya wengi Barani Afrika kwa kuvunjilia mbali miundo inayochangia uwepo wa dhambi na mambo yote yanayochangia umaskini na nyanyaso katika utu na heshima ya binadamu.

Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar linaendelea kuhimiza umuhimu wa kuenzi Injili ya Uhai kwa watoto, familia pamoja na kuhakikisha kwamba, watu wanapata chakula na lishe bora; huduma bora ya elimu na afya na kwamba, elimu inachangia kwa namna ya pekee katika kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na upatanisho kati ya watu.

SECAM kwa namna ya pekee, imewakumbuka pamoja na kuonesha mshikamano wake na nchi za Kiafrika ambazo kwa sasa zinakabiliana na vita, chuki na madhulumu ya kidini na kisiasa hasa: DRC, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, Nigeria, Misri, Mali na baadhi ya sehemu ambazo mambo si shwari sana. SECAM inakumbusha kwamba, rasilimali na utajiri wa Bara la Afrika unapaswa kuwa ni kwa ajili ya mafao ya wengi, ustawi na maendeleo ya wananchi wa Bara la Afrika na wala si kwa ajili ya kikundi cha watu wachache na familia zao tu!

SECAM inasema ukabila, udini na umajimbo ni mambo ambayo yamepitwa na wakati Barani Afrika na badala yake, wananchi wajikite katika kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na utulvu na kwamba, kuna haja ya kuendelea kujikita katika dhamana ya Uinjilishaji wa kina, kama sehemu mchakato unaopania toba na wongofu wa ndani, Yesu Kristo akipewa kipaumbele cha kwanza katika uhalisia wa maisha.

Ujumbe wa SECAM umehaririwa na
Padre Richard Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.