Rais Mugabe aibuka kidedea, Tsvangirai asusia matokeo!
Tume ya Uchaguzi Zimbabwe imemtangaza Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe kuwa mshindi
katika uchaguzi mkuu uliofanyika kunako tarehe 31 Julai 2013. Rais Mugabe ameibuka
na ushindi kwa asilimia 61% ya kura zote halali zilizopigwa na kumshinda mpinzani
wake Waziri mkuu wa zamani Morgan Tsvangirai aliyepata asilimia 34% ya kura zote halali
zilizopigwa.
Rais Mugabe na chama chake cha ZANU-PF wamepata viti 160 vya
wabunge na Chama cha Tsvangirai, MDC kimejipatia viti 49. Bwana Tsvangirai anapinga
matokeo ya uchaguzi mkuu kutokana na kasoro nyingi zilizojitokeza katika mchakato
mzima na kwamba, kuanzia sasa wataanza kwenda mitaani kupinga matokeo ya uchaguzi
mkuu. Viongozi kadhaa kutoka Afrika wamemtumia Rais Mugabe salam za pongezi kwa kuibuka
kidedea katika uchaguzi huu ambao sasa unaonekana kuwa na utata!