Mkiandamana na Yesu pamoja na Mtakatifu Gaetano, nendeni mkawahudumie maskini!
Baba Mtakatifu Francisko ametuma ujumbe wa matashi mema kwa njia ya video kwa waamini
na watu wote wenye mapenzi mema nchini Argentina katika kumbu kumbu ya Maadhimisho
ya Siku kuu ya Mtakatifu Gaetano, msimamizi wa Argentina, inayoadhimishwa kila mwaka
ifikapo tarehe 7 Agosti. Maadhimisho ya Mwaka 2013 yanaongozwa na kauli mbiu "Yesu
pamoja na Mtakatifu Gaetano twende kuwahudumia maskini".
Baba Mtakatifu anasema,
licha ya umbali anapenda kutumia fursa hii kukutana nao, ili kwa pamoja waweze kukutana
na Yesu pamoja Mtakatifu Gaetano ili kuwahudumia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni
mwa Jamii. Hawa ni watu wanaohitaji kushirikishwa na kuonjeshwa huruma na upendo katika
shida na mahangaiko. Hapa kuna haja ya kukutana nao ana kwa ana, kama kielelezo makini
cha maisha na mafundisho kutoka kwa Kristo, ambaye daima alijitosa kimasomaso kwa
ajili ya maskini bila hata ya kujibakiza hata kidogo.
Hata katika kutoa sadaka
kwa maskini, kuna haja ya kujenga utamaduni wa kuwaangalia, kuwajali na kuwathamini
kama binadamu, changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuibua,kujenga
na kukuza utamaduni wa kukutana na watu wanaowazunguka. Waamini wakumbuke kwamba,
kuna watu wengine wanateseka pengine kuliko wao na kwamba, ni watu wanaohitaji kuonja
huruma na upendo.
Baba Mtakatifu anawashukuru waamini na wananchi wa Argentina
katika ujumla wao kwa kumsikiliza anapoendelea kuwahimiza kujenga dhana ya kukutana
daima wakiwa wameandamana na Yesu pamoja na Mtakatifu Gaetano. Kwa njia ya ushuhuda
huu wa maisha, wanaweza kuwa kweli ni kikolezo na mvuto wa toba na wongofu wa ndani.
Mtu ambaye amekutana na kumkirimia mhitaji zaidi, moyo wake unakuwa na kupanuka kutokana
na upendo.
Baba Mtakatifu anahitimisha ujumbe huu kwa njia ya video ambao
umerushwa na vyombo mbali mbali vya habari nchini Argentina kwa kuwasihi ili waendelee
kumwombea katika maisha na utume wake!