2013-08-07 11:21:58

Kura ya marudio nchini Mali ni hapo tarehe 11 Agosti 2013


Wananchi wa Mali wanajipanga tena kurudia uchaguzi mkuu hapo tarehe 11 Agosti 2013 baada ya wale waliokuwa kwenye kinyang'anyiro cha uchaguzi mkuu uliofanyika hapo tarehe 28 Julai 2013 kushindwa kupata asilimia 50%. Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki nchini Mali ambalo lilitoa waangalizi 153 wakati wa uchaguzi mkuu awamu ya kwanza. Caritas Mali inashauri kufanyike maboresho katika mchakato wa uchaguzi nchini humo, kwa ajili ya kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na utulivu.

Tume ya uchaguzi nchini Mali inapaswa kujipanga vyema zaidi ili kutoa habari kwa ajili ya wananchi wakati wa machakato mzima wa upigaji kura. Lengo ni kurahisisha zoezi zima la upigaji kura, kwani katika awamu ya kwanza ya uchaguzi, wananchi wengi walijikuta hawafahamu vituo vyao vya kupigia kura. Mali inapaswa kuwa na Tume huru ya uchaguzi itayoshirikiana na taasisi nyingine ili uchaguzi uweze kuwa ni huru na kweli.

Wagombea uchaguzi pamoja na wananchi wa Mali wanaendelea kuhamasishwa ili kulinda na kudumisha amani na utulivu wakati na baada ya matokeo ya uchaguzi mkuu kutangazwa. Mali imekuwa katika mgogoro wa kivita kuanzia Januari, 2013.







All the contents on this site are copyrighted ©.