Kanisa Katoliki nchini Madagascar lakanusha taarifa kwamba, CRS inatoa dawa za kuzuia
na kudhibiti mimba kinyume cha mafundisho ya Kanisa Katoliki!
Askofu Mkuu Odon Razanakolona wa Jimbo kuu la Antananarivo, Madagascar, amekanusha
madai kwamba Shirika la Misaada la Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, CRS lilihusika
kwenye ugavi wa dawa za kukinga na kutoa mimba nchini Madagascar.
Askofu Mkuu
Razanakolana aliyasema hayo alipokuwa akizungumza kwenye simu na askofu Gerald Kicanas,
mwenyekiti wa bodi ya CRS pamoja na wajumbe wengine wa CRS na Baraza la Maaskofu Katoliki
Marekani.
Askofu mkuu Razanakolona ni kiongozi wa pili wa Kanisa katika kipindi
cha siku chache kukanusha madai hayo yaliyochapishwa hivi karibuni na Taasisi ya Kimataifa
cha Utafiti wa Idadi ya watu. Askofu mkuu Razanakolona anasema, alishangazwa na kuona
akinukuliwa kwenye ripoti ya utafiti wa Taasisi na kwamba ana uhakika kabisa CRS hufuata
Mafundisho ya Kanisa na haijajishughulisha na ugawaji wa dawa za kukinga na kutoa
mimba.
Hivi karibuni, Askofu Mkuu Desire Tsarahazana wa Jimbo kuu la Toamasina,
ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Madagascar alionyesha mshikamano
wake na shirika la CRS huku akisema kwamba, kwenye jimbo lake, CRS huendesha shughuli
zake kulingana na Mafundisho Jamii ya Kanisa Katoliki.
Ripoti ya uchunguzi
wa shughuli za shirika la CRS nchini Madagascar iliyochapishwa na Taasisi ya Utafiti
wa idadi ya watu duniani, inadai kwamba, Shirika hilo, linaloendeshwa na misaada kutoka
Kanisa Katoliki Marekani, lilikuwa linagawa dawa za kuzuia na kutoa mimba, kinyume
cha Mafundisho na msimamo wa Kanisa. Hata hivyo, madai haya sasa yamekanushwa na
Kanisa Katoliki nchini Madagascar.