Benki ya Vatican katika utekelezaji wa mikakati yake kwa kuzingatia ukweli, uwazi,
tija na ufanisi
Baba Mtakatifu Francisko akiziungumza na waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara
wake amekazia umuhimu wa Benki ya Vatican kutekeleza dhamana na majukumu yake kwa
kuzingatia: maadili, ukweli na uaminifu. Benki ya Vatican, IOR yaani “Istituto per
le Opere di Religione” ilianzishwa tarehe 27 Juni 1942 na Waraka wa Kipapa, ikapewa
jukumu la kuratibu masuala ya fedha kwa Vatican na wadau wake ndani ya Kanisa Katoliki
sehemu mbali mbali za dunia.
Chimbuko la
Benki hii ni wazo lililotolewa na Baba Mtakatifu Leo wa XIII kunako mwaka 1887, aliyeanzisha
tume kwa ajili ya mafao ya Kanisa. Benki hii iliendelea kutekeleza majukumu yake,
ikapambana na changamoto na kinzani mbali mbali.
Kunako Mwaka 1990 Mwenyeheri
Yohane Paulo II akafanya marekebisho makubwa katika Katiba ya Benki ya Vatican, ili
iweze kulinda na kuratibu mali na fedha ambazo zimekabidhiwa kwa Taasisi hii ya fedha
kwa ajili ya shughuli za kidini na matendo ya huruma. Wafanyakazi na taasisi zinazotekeleza
wajibu wake mjini Vatican zinaweza kuweka na kutunza fedha katika Benki hii. Ni Benki
inayotekeleza wajibu wake kwa ajili ya Kanisa la Kiulimwengu kwa kulinda amana, rasilimali
ya Kanisa pamoja na kutoa huduma za kibenki sehemu mbali mbali za dunia.
Ni
Benki inayotoa huduma pia kwa: majimbo, Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, Taasisi
za Kanisa Katoliki pamoja na wafanyakazi wa Vatican walioenea sehemu mbali mbali za
dunia bila kuwasahau wanadiplomasia. Benki ya Vatican inatekeleza dhamana yake mjini
Vatican peke yake.
Kutokana na takwimu zilizotolewa hadi kufikia mwishoni mwa
Mwaka 2012, Benki ya Vatican ilikuwa inahudumia taasisi 5,200 za Kanisa Katoliki:
yaani: Vatican na taasisi zake, Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume pamoja na Majimbo
ambayo kwa pamoja yanaunda asilimia 85% ya akaunti zilizoko Benki ya Vatican, zenye
thamani ya Euro Billioni 6.0 kati ya Euro Billioni 7.1 zinazohifadhiwa kwenye Benki
ya Vatican.
Takwimu zinaonesha kwamba, kuna jumla ya wateja 13, 700: hawa ni
Makleri, Watawa, Wafanyakazi pamoja na wafanyakazi wastaafu wa Vatican wanaopokea
mishahara na pensheni zao za uzeeni pamoja na wanadiplomasia wanaowakilisha nchi na
taasisi mbali mbali za kimataifa mjini Vatican. Kundi hili linaunda asilimia 15% ya
akaunti za Benki ya Vatican zenye thamani ya Euro Billioni 1.1 kati ya Euro Billioni
7.1. Benki hii inaendelea kufuata: maadili, sheria na kanuni za Vatican na zile za
Kimataifa kwa kuzingatia ukweli, uaminifu na uwazi.
Benki ya Vatican kwa sasa
inaendelea kufanyiwa marekebisho makubwa kwa kusoma alama za nyakati pamoja na kukabiliana
na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika masuala ya fedha, utandawazi na maendeleo
ya sayansi na teknolojia.