2013-08-06 11:47:19

Umoja wa Vijana Wakatoliki Hispania wanachangamotishwa kuwa Wamissionari na Wainjilishaji!


Vijana wanaitwa na kutumwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia, ndiyo kauli mbiu iliyoongoza Maadhimisho ya Mkutano mkuu wa Chama cha Vijana Wakatoliki Hispania, uliohitimishwa hivi karibuni katika Jimbo kuu la Madrid, Hispania. Vijana zaidi ya mia sita kutoka katika majimbo 44 yanayounda Kanisa Katoliki nchini Hispania walihudhuria.

Askofu mkuu Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji Mpya, aliwataka vijana kuzamisha mizizi ya imani katika maisha yao, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa uwepo wa Kristo. Chama cha Vijana Wakatoliki, kimsingi ni Jumuiya inayowaunganisha: watoto, vijana na wazee kuwa kama Parokia inayojipambanua katika mchakato wa Uinjilishaji mpya.

Ni wajibu wa Chama cha Vijana Wakatoliki kwenda Maparokiani ili kuhamasisha ari na moyo wa Kimissionari, kwa kushirikiana na wote, ili Parokia na Jumuiya za Waamini zijisikie kuwa ni sehemu ya utume wa Kimissionari zinazotumwa Kuinjilisha. Waamini walei wanaendelea kuhamasishwa na Mama Kanisa kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yanayojikita kwa kukutana na Yesu, ili kuwashirikisha wengine ile furaha ya imani.

Viongozi wa Kanisa nchini Hispania wanasema, athari za myumbo wa uchumi kimataifa na kimaadili, iwe ni fursa makini kwa waamini kutoa mwanya kwa Roho Mtakatifu ili kuwasaidia kujenga na kudumisha: utamaduni wa kusimama kidete kulinda na kutetea zawadi ya uhai; kujenga na kuimarisha moyo na ari ya kusali daima pamoja na kuendelea kushiriki kikamilifu katika Maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa. Misingi ya maadili na utu wema ipewe msukumo wa pekee kama kielelezo cha toba na wongofu wa ndani unaopania kushuhudia kweli za Kiinjili.

Umoja wa Vijana Wakatoliki Hispania hauna budi kushirikiana kwa karibu zaidi na viongozi wa Kanisa mahalia. Katika kipindi cha miaka minne, vijana hawa wanapenda kudumisha tasaufi ya kitume inayojikita kwa Kristo; ni mwaliko na changamoto kwa vijana kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.

Vijana wanahamasishwa kujenga utamaduni wa kukutana na kuzungumza na Yesu kwa njia ya Neno la Mungu, Tafakari ya kina na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu sanjari na ushiriki makini wa Maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa. Vijana wanaendelea kuhimizwa kujitosa kimasomaso katika azma ya Uinjilishaji mpya kwa njia ya ushuhuda wa maisha, unaopania kuyatakatifuza malimwengu.

Maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni, wanapaswa kuwa ni kipaumbele cha mikakati ya shughuli za kichungaji zitakazotekelezwa na Umoja wa Vijana Wakatoliki nchini Hispania katika kipindi cha miaka minne kuanzia sasa!







All the contents on this site are copyrighted ©.