2013-08-06 08:28:12

Mateso na mahangaiko ya watu kutokana na vita ni matokeo ya dhambi ya mwanadamu na mwendelezo wa utawala wa Shetani!


Ilikuwa ni tarehe 6 Agosti 1945, miaka 68 iliyopita, bomu la kwanza la atomic liliporushwa mjini Hiroshima, nchini Japana na kusababisha madhara makubwa. Ni maneno ya Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani wakati alipokuwa anazungumza na viongozi wa dini mbali mbali nchini Japan kama sehemu ya Maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Miaka 68 tangu mji wa Hiroshima ulipopiga bomu.

Hata leo hii, kuna mamillioni ya watu wanaoendelea kuteseka kutokana na madhara ya vita, lakini watu wanaziba masikio kana kwamba, hakuna kinachoendelea. Kunako mwaka 1981, Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili alipotembelea Japan alisema kwamba, mateso na mahangaiko ya watu kutokana na vita ni matokeo ya dhambi na mwendelezo wa kazi ya Shetani. Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, umilikaji na matumizi ya silaha za atomic unaweza kusababisha madhara makubwa kwa binadamu. Mtu anapojikweza kupita kiasi anaweza kusababisha maafa.

Watu binafsi na Jamii mara nyingi anasema Kardinali Turkson, zinashawishika kujikita katika uchoyo unaosbabisha chuki, badala ya kuwakumbatia na kuwasaidia wale wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Changamoto kubwa kwa sasa ni kuwakumbatia wale wasiokuwa nacho; kuwasaidia badala ya kuwalaani; kwa pamoja, Jamii itoke kifua mbele ili kukabiliana na miundo na mambo ambayo yanasababisha ukosefu wa haki, kinzani na migogoro ndani ya Jamii.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, hakuna amani ya kweli, maendeleo, ustawi, utulivu na amani, katika Jamii ambamo, sehemu ya wananchi wake wanatengwa na kusukumizwa pembezoni mwa Jamii. Amani ya kweli inawakumbatia wote na kuwaingiza katika maisha ya Kijamii. Hii ndiyo mantiki ya Fumbo la Msalaba ambalo ni kielelezo makini cha ushindi wa Kristo dhidi ya dhambi na mauti.







All the contents on this site are copyrighted ©.