Kanisa linapaswa kutekeleza shughuli zake za kichungaji kitaaluma, kwa kuzingatia
maadili, ukweli na uwazi!
Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari
wakati akirejea kutoka Brazil kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani
kwa Mwaka 2013 alikazia umuhimu wa taasisi za Kanisa kutekeleza majukumu yake kwa
kuzingatia misingi ya maadili, ukweli, uwazi na uaminifu.
Hivi karibuni, Baraza
la Maaskofu Katoliki Rwanda kwa kushirikiana na Shirika la Misaada la Baraza la Maaskofu
Katoliki Marekani, liliendesha semina maalum kwa ajili ya wafanyakazi wa Idara za
Baraza la Maaskofu Katoliki Rwanda kuhusu matumizi sahihi na makini ya rasilimali
ya Kanisa kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa Kanisa Katoliki nchini Rwanda.
Katika
hotuba yake ya ufunguzi, Padre Cèlestin Hakizimana, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu
Katoliki Rwanda alifafanua kuhusu utekelezaji wa mikakati ya shughuli za kichungaji
za Baraza la Maaskofu Katoliki Rwanda kuanzia mwaka 2008 hadi mwaka 2017 zinazopania
Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kanisa Katoliki
nchini Rwanda linataka kutekeleza shughuli zake za huduma kwa watu wa Mungu kitaalamu
wala si kwa kubabaisha.
Padre Hakizimana amewakumbusha wanasemina kuhusu Mafundisho
Jamii ya Kanisa na Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki juu ya matumizi sahihi ya rasilimali
ya Kanisa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Watu wa Mungu. Wafanyakazi wa Kanisa
wanapaswa kuzingatia kanuni, maadili, ukweli na uwazi katika matumizi ya rasilimali
ya Kanisa, vinginevyo hata wao wanaweza kujikuta wakitumbukia katika kashfa ya ufisadi
na ubadhilifu wa mali ya Kanisa kama inavyojitokeza katika Jamii nyingi kwa sasa.