2013-08-05 10:03:57

Utajiri wa kweli unajikita katika upendo unaowashirikisha na kuwahudumia jirani!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Tafakari ya Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili, tarehe 4 Agosti 2013, alimshukuru Mungu kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana wakati wa Maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani huko Rio de Janeiro. Hii imekuwa ni zawadi kubwa kwa Brazil, Amerika ya Kusini na duniani kote! Hii ni awamu nyingine tena katika hija ya vijana wanaotembeza Msalaba wa Kristo sehemu mbali mbali za dunia.

Maadhimisho ya Siku za Vijana Duniani si moto wa mabua! Bali ni hija iliyoanzishwa na Mwenyeheri Yohane Paulo II kunako mwaka 1985. Aliwakabidhi vijana Msalaba akiwatuma kuutembeza duniani kote na Yeye angewafuata baadaye. Hija hii imeendelezwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita na hatimaye, Papa Francisko anasema kwa neema ya Mwenyezi Mungu ameweza hata yeye kushiriki katika Maadhimisho haya kwa awamu hii.

Baba Mtakatifu Francisko ameuambia umati mkubwa wa waamini na mahujaji uliokuwa umefurika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican licha ya jua kali kwamba, vijana wanamfuata Yesu na wala si Khalifa wa Mtakatifu Petro, kwani yeye anawajibu wa kuwasindikiza katika hija hii ya imani na matumaini. Baba Mtakatifu anawashukuru kwa dhati kabisa vijana wote walioshiriki katika Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani.

Baba Mtakatifu anamshukuru Mungu aliyemwezesha kukutana na Wachungaji wa Familia ya Mungu, Viongozi wa Serikali nchini Brazil pamoja na vijana waliokuwa wanajitolea. Anasema, hana cha kuwalipa, isipokuwa Mwenyezi Mungu mwingi wa neema na baraka aweze kumkirimia kila mtu aliyejitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kufanikisha Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani. Amewashukuru pia wananchi wa Brazil kwa moyo wao wa upendo na ukarimu waliomwonesha na kumshirikisha wakati wa hija yake ya kichungaji nchini Brazil.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuungana naye ili kuwaombea vijana walioshiriki katika Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani huko Brazil, kuweza kumwilisha mang'amuzi na uzoefu waliojichotea katika maamuzi ya maisha, daima wakiwa tayari kuitikia wito binafsi kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Baba Mtakatifu anasema, Liturujia ya Neno la Mungu inaonesha ubatili na utupu ambao vijana wanaweza kukumbana nao katika maisha yanayowazunguka. Kwa bahati mbaya vijana ndio waathirika wakuu. Lakini vijana hawa wakithubutu kukutana na Yesu kwa njia ya familia kubwa ambayo ni Kanisa, atawajaza furaha mioyoni mwao, kwani Kristo ni chemchemi ya maisha ya kweli na fao kuu lisiloharibika kamwe. Haya ndiyo yaliyojidhihirisha katika nyuso za vijana waliokuwa mjini Rio de Janeiro.

Baba Mtakatifu anasema, mang'amuzi haya hayana budi kuwasaidia vijana kupambana na ubatili wa maisha, unaoendelea kujitokeza kila siku kwa kujikita katika faida na kile ambacho mtu anamiliki, mambo yanayowatumbukiza vijana katika ulaji wa kupindukia.

Neno la Mungu linawachangamotisha waamini na watu wenye mapenzi mema kutosimika furaha yao katika mali, bali katika upendo unaowawajibisha kuwashirikisha na kuwasaidia wengine. Kwa mtu mwenye mang'amuzi ya namna hii, hawezi kamwe kuogopa kifo kama ilivyojitokeza kwenye Injili ya Luka, 12:19-20 kwani ni mtu ambaye moyo wake umesheheni amani.







All the contents on this site are copyrighted ©.