2013-08-05 07:45:00

Kanisa linavyowekeza katika majiundo ya vijana duniani


Ni muujiza uliowezeshwa kwa msaada wa Papa mstaafu Benedikto XVI pamoja na mchango wa fedha kutoka Shirika la msaada kwa Kanisa hitaji. Ndiyo maneno aliyoyatumia Kardinali Christoph Schònborn, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Vienna kusimulia aliyoyashududia alipokuwa huko Rio de Janeiro, nchini Brazil katika Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya 28 ya Vijana Duniani iliyoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko. RealAudioMP3

Kardinali Schònborn hasa alikuwa akiongelea kile alichokiita “muujiza” wa Youcat, yaani Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki kwa ajili ya Vijana iliyoanzishwa mnamo 2011 wakati wa Maadhimisho ya Diku ya Vijana Duniani, iliyofanyika Jimbo kuua la Madrid. Youcat kwa sasa ndio mradi mkubwa zaidi wa Kikatoliki ulimwenguni unaowahusisha wahariri wa vitabu, umetafsiriwa kwa zaidi ya lugha 27 na unawafikia vijana wengi kwa ajili ya majiundo yao kiimani, kisakramenti, kiutu na katika maisha ya sala. Kwa maneno mengine, huu ni muhtasari wa Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki mahususi kwa ajili ya vijana.

Wakati wa maadhimisho ya siku ya Vijana ulimwenguni mwaka 2013, Shirika la Msaada kwa Kanisa Hitaji liliweza kugharimia nakala milioni 1.5 za Youcat kwa vijana walioshiriki katika Maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani huko Brazil.

Kardinali Schònborn anamshukuru Papa Mstaafu Benedikto XVI kwa kuubariki mradi huu ambao ni sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji Mpya miongoni mwa Vijana wa Kanisa Katoliki. Vijana wanahamasishwa kuwa ni wadau wakuu wa Uinjilishaji miongoni mwa vijana wenzao. Kardinali Schonborn anapongeza kazi kubwa inayofanywa na Shirika la Kipapa la Msaada kwa Kanisa Hitaji, kwa ajili ya kufanikisha utume huu miongoni mwa vijana.









All the contents on this site are copyrighted ©.