2013-08-05 08:38:12

Familia ni shule ya kwanza ya maadili na utu wema!


Ndugu zangu wapendwa tuanze tafakari yetu ya leo kwa kuongozwa na maneno ya busara kutoka kwa Mababa wa Mtaguso wa mkuu wa Pili wa Vatican katika tamko lao kuhusu elimu ya Kikristo. Mababa wa Mtaguso katika kifungu namba 3 walisema “familia ni shule ya kwanza ya fadhila za kijamii ambazo kila jamii inahitaji”. RealAudioMP3
Kwa neema za Mungu zinazopatikana katika Sakramenti ya ndoa, watoto wanaanza kujifunza kuanzia miaka yao ya mwanzo kumpenda Mungu kulingana na imani wanayopokea katika Ubatizo, kumuabudu Yeye, na kuwapenda jirani zao.
Tunapobatizwa kila mmoja wetu anashiriki katika kazi kuu tatu za Kristu yaani unabii kwa kumshuhudia Kristo kwa maneno na matendo yetu; ukuhani kwa kujitoa kama sadaka kwa wenzi wetu, familia yetu na taifa zima la Mungu; na ufalme kwa kuwaongoza wengine kwa Mungu kwa mifano bora ya maisha yetu. Wanandoa kama viongozi wa familia wanapokea wajibu huo kwa namna ya pekee zaidi kwao binafsi na kwa watoto wao.
Ni katika familia wanandoa na watoto wanaweza kujifunza kumcha Mungu, kutambua maana ya kupenda wanapoonja jinsi wanavyopendwa Mungu, wanavyopendana wao kwa wao, wanavyowapenda watoto na wanavyowapenda majirani zao; watoto wanaweza kujifunza pia maana ya msamaha jinsi wanavyoonja msamaha wa Mungu wanapomkosea, jinsi wazazi wanavyosameheana wanapokoseana, jinsi wanavyowasameha watoto wao pale wanapokosea na jinsi wanavyowasamehe majirani zao pale wanapowakosea.
Maisha ya familia yana mahusiano makubwa na maisha ya jamii kwa ujumla kwasababu familia inaishi ndani ya jamii. Hivyo tunapozunguzia familia ni vyema tukapeleka fikra zetu kwenye familia asilia ambayo ni Baba, Mama na Watoto na pili familia nzima ya Mungu ambayo inatuunganisha sisi binadamu wote tulioumbwa kwa sura na mfano Mungu. Kama wanafamilia kwa ujumla, tukumbuke kuwa Wahenga wetu walikuwa na maneno na misemo mingi ambayo ilikuwa na busara nyingi katika kutoa elimu kwa jamii.
Tunaposonga mbele katika ulimwengu huu wa Sayansi na Teknolojia tutazame pia tumetoka wapi kusudi yale mazuri tusiyaache nyuma bali tuyachukue na kusonga nayo mbele. Kwa mfano, wahenga wetu walisema, “Asiyefunzwa na mamaye, atafunzwa na ulimwengu”.
Nilipokuwa ninaitafakari methali hii, niliona kuwa imejaa hekima nyingi ambapo ina pande tatu za msingi; kwa upande mmoja inalalenga jukumu la wazazi katika kutoa malezi bora kwa watoto; upande mwingine watoto kuwatii na kuwaheshimu wazazi kwani wakiwa wakaidi ulimwengu utawafanza; na upande wa tatu ni ulimwengu lakini mpaka pale tunapouchia ulimwengu utoe malezi ya msingi kwa mtoto tayari tunakuwa tumeruka hatua muhimu ya malezi ambayo yalitakiwa yafanyike katika ngazi ya familia.
Pia tuendelee kukumbuka busara za wahenga wetu kuwa “uchungu wa mwana aujuaye mzazi”. Malezi ambayo tutauchia ulimwengu umpatie mtoto, hayawezi kuwa sawasawa na malezi ya wazazi.
Zaidi ya elimu inayopatika katika familia, inatupasa tukumbuke kuwa wana familia nzima ya Mungu tunawajibika katika kutoa mifano bora kwa watu wanaotuzunguka kwa lengo ya kujenga familia na jumuiya zenye mapendo, haki na amani .
Tukijaribu kutafakari maisha yetu ya ya kifamilia na kijamii tutakuja kugundua kuna mambo mengi yanayotokea. Mengine ni mambo mazuri na mengine hayapendezi kwasababu hayadhihirishi upendo kwa nafsi zetu wenyewe, kwa Mungu na kwa jirani zetu.
Mara nyingi sisi binadamu, mambo yanapokwenda vizuri katika mazingira Fulani tunafurahia na pia tunapenda hata kushiriki katika kujipatia sifa, lakini mambo yanapokwenda vibaya tunatafuta sehemu ya kutupia lawama na sisi kujiweka pembeni kama kwamba hatuhusiki kabisa.
Katika matukio mbali mbali mbali yanayotokea, ninawaomba leo hii tujaribu kutafakari heshima ya utu katika familia zetu tukitazama mauaji ya Albino wasiokuwa na hatia yoyote kutokana na imani za kishirikina na ulafi wa mali ambazo tukifa tunaviacha vyote!
Ni watu wangapi wanao uwawa kutokana utoaji mimba na mauaji ya bidanamu wenzetu wengi wasiokuwa na hatia kutokana na sababu za ubinafsi mambo ambayo yanatupelekea kunakosa amani katika familia zetu kwasababu damu za watu zisizokuwa na hatia zinatulilia! Je, hao wanaofanya vitendo hivyo hawajatokea kwenye wanafamilia zetu au jamii zetu?
Mwaka huu wa imani sisi wanafamilia ya Mungu tunaalikwa kutafari kwa kina wajibu wetu katika familia na taifa zima la Mungu.
Katika kutimiza wajibu wetu kwa Mungu, kwa familia zetu na kwa taifa zima la Mungu, hatuwezi kufanikiwa vizuri kwa nguvu zetu wenyewe. Tunahitaji hekima ambayo ni zawadi kutoka kwa Mungu. Tuige mfano mfalme Sulemani aliyepewa uhuru wa kuchagua zawadi yoyote anayopenda katika maisha naye akachagua hekima ya kupambanua jema na baya (1 Wafalme 3:9). Katika Kitabu cha (Mithali 9:10) tunaambiwa kuwa mwanzo wa hekima hiyo ya kweli ni kumcha Mungu.
Wapendwa wanafamilia ya Mungu, huu ni wakati muafaka wa kutafakari tena mahusiano yetu na Mungu, familia zetu na jamii kwa ujumla, na pale tulipokuwa tumevunja mahusiano hayo kwa namna yoyote tufanye toba ya kweli na kuanza maisha mapya kusudi tuwe mashahidi wa kweli wa Injili ya Kristu katika familia zetu na Taifa zima la Mungu.
Makala hii imeandaliwa na Padre Titus Nkane, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.