2013-08-03 07:42:51

Mikakati ya shughuli za kichungaji Amerika ya Kusini, ili kukabiliana na changamoto zilizopo!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kichungaji nchini Brazil, tarehe 28 Julai 2013, alipata pia fursa ya kukutana na kuzungumza na Maaskofu 45 wanaounda Sekretarieti ya Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu katoliki Amerika ya Kusini na Caribbeni, CELAM.

Baba Mtakatifu katika mazungumzo yake, alijikita zaidi katika Maadhimisho ya Mkutano wa Tano wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini uliofanyika mjini Aparecida. Kwa mara ya kwanza, mkutano huo uliadhimishwa kwenye Madhabahu ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya asili wa Aparecida nchini Brazil., hapo Mwezi Mei, 2007.

Baba Mtakatifu alianza hotuba yake iliyosheheni changamoto kwa Shirikisho la Baraza la Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini, kwa kuzungumzia kwanza kabisa mihimili iliyobainishwa na Mababa wa Aparecida wakati wa mkutano wao. Kwanza, ulikuwa ni ushiriki wa Makanisa mahalia kwa njia ya: Sala, Tafakari, Ibada na Maadhimisho mbali mbali yaliyowasindikiza Maaskofu wakati wa mkutano wao huko Aparecida.

Mkutano huu ulianzisha mchakato endelevu uliokuwa unapania kuhakikisha kwamba, Kanisa linaendeleza dhamana na utume wake wa kutangaza Injili ya Kristo huko Amerika ya Kusini. Baba Mtakatifu amewakumbusha Maaskofu hao kwamba, huu ulikuwa ni mkutano wao wa kwanza kufanyika chini ya ulinzi na usimamizi wa Bikira Maria wa Aparecida.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, utume na dhamana ya Kanisa Amerika ya Kusini una mielekeo mikuu miwili; kwanza kabisa ni mbinu mkakati wa shughuli mbali mbali za kimissionari zinazotekelezwa na Mama Kanisa Amerika ya Kusini. Pili ni mwelekeo wa utekelezaji wa utume huu katika uhalisia wa maisha ya Makanisa mahalia.

Utekelezaji wa majukumu haya unahitaji mabadiliko ya miundo mbinu ya Kikanisa kutoka katika mfumo wa sasa na kuanzisha mifumo mipya kabisa, ili kuliwezesha Kanisa kusonga mbele kwa imani na matumaini zaidi. Huu ni mchakato unaojikita katika undani wa maisha ya waamini, unaowaalika waamini kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu, kwa kujenga na kuimarisha ndani mwao ari na moyo wa kimissionari.

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake kwa Maaskofu wa Sekretarieti ya Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini, amebainisha changamoto kuu mbili zinazolikabili Kanisa katika mazingira ya Amerika ya Kusini; mosi ni Utume wa Kimissionari unaolichangamotisha Kanisa kufanya mabadiliko ya ndani katika maisha na utume wake, tayari kutoka kifua mbele ili kujadiliana na ulimwengu unaolizunguka.

Katika dhamana hii, kuna vishawishi vinavyoweza kujitokeza kwa kuugeuza Ujembwa Injili kuwa na mwelekeo na sera za kisiasa; kishawishi cha kutaka kuifasiri Injili nje ya Injili na uhalisia wa maisha na utume wa Kanisa. Kishawishi kingine ni kulifanya Kanisa kuwa kama mashine ya kutekeleza miradi ya maendeleo kiasi cha kuligeuza Kanisa kuwa kama NGO fulani hivi.

Katika mwelekeo huu, taalimungu inayoibuliwa ni ile ya utajiri na ufanisi ambayo hatima yake inajikita katika mikakati ya shughuli za kichungaji zinazofanywa na Mama Kanisa. Baba Mtakatifu anasema, kishawishi kingine kikubwa kinachoendelea kujionesha Amerika ya Kusini ni hali ya Makleri kuona kwamba, maisha na utume wao ni kama ajira, hali inayoonesha kwa namna ya pekee ukosefu wa ukomavu na uhuru wa Kikristo hata miongoni mwa waamini wengi Amerika ya Kusini.

Baba Mtakatifu akizungumza na Maaskofu wa CELAM, ameonesha dira na mwongozo unaopaswa kutekelezwa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Amerika ya Kusini. Jambo la kwanza ni kujenga na kuimarisha Utume wa Kimissionari, changamoto iliyotolewa na Mababa wa Aparecida. Huu ndio utashi wa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya Kanisa la Amerika ya Kusini kwa nyakati hizi, licha ya kinzani na changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza. Utume wa Kimissionari ni ari na mwelekeo endelevu, daima unaojitahidi kusoma alama za nyakati.

Jambo la pili anasema Baba Mtakatifu ni kutambua kwamba, Kanisa ni Taasisi iliyoanzishwa na Kristo, ambayo inahamasishwa kutoka kwenda kutangaza Injili ya Kristo hadi miisho ya dunia na wala isijitafute yenyewe, vinginevyo, taasisi hii itakuwa ni kama mradi au NGO. Kwa mwelekeo huu, Kanisa linakuwa si tena mchumba mwaminifu wa Kristo; Mhudumu wa Neno la Mungu na Mafumbo Matakatifu, linajikuta likiwa ”Askari na Msimamizi”.

Baba Mtakatifu Francisko anakumbushia kwamba, Mkutano wa Aparecida, ulilichangamotisha Kanisa Amerika ya Kusini kuwa ni: Mchumba mwaminifu wa Kristo, Mama na Mtumishi mwaminifu; Mkolezaji wa imani na wala si mdhibiti wa imani miongoni mwa waamini.

Jambo la tatu anaendelea kubainisha Baba Mtakatifu Francisko ni mikakati miwili ya shughuli za kichungaji iliyoibuliwa na Mababa wa Aparecida. Mikakati hii inatambua upekee wa Injili inayoweza kulisaidia Kanisa kujipima ikiwa kama linaishi ile dhamana ya Umissionari, kwa kuwa karibu na kukutana na waamini katika hija ya maisha yao ya kiroho na kiutu. Hizi ni njia ambazo Mwenyezi Mungu amezionesha katika historia ya ukombozi, ili kuwachangamotisha waamini kujisikia kuwa ni sehemu ya maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu anasema, kipimo madhubuti ikiwa kama Kanisa liko na linakutana na Waamini wake ni Mahubiri.

Jambo la tano, anasema Baba Mtakatifu ni Maaskofu kutekeleza wajibu na dhamana yao ya kuongoza Familia ya Mungu, ili kuonesha dira na njia makini ya kufuata na wala si kutawala. Maaskofu wanapaswa kuwa ni wachungaji wema na waaminifu, watu ambao wanatambua shida na mahangaiko ya watu wao. Askofu ni kiongozi ambaye hana budi kuwa kweli na fadhila ya: uvumilivu, huruma, upole na unyenyekevu.

Watu ambao wanapenda kukumbatia ufukara na maisha ya kiasi, wakiwa huru katika kutumia mali na rasilimali ambayo imewekwa mbele yao na Mama Kanisa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Familia ya Mungu. Maaskofu waoneshe unyofu wa ndani na wala kamwe wasijisikie kuwa ni ”Wafalme na miungu wadogo wanaoabudiwa”. Ni watu ambao wanajitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa bila ya kumezwa na malimwengu.

Askofu awe ni kiongozi anayejitaabisha kujenga na kuimarisha umoja, upendo na mshikamano miongoni mwa Familia ya Mungu. Asimame kidete kuwalinda waamini wake dhidi ya hatari zinazoweza kujitokeza katika safari ya maisha yao ya kiroho na kiutu, lakini zaidi, kwa wale wanaotaka kuwapora matumaini kutoka katika undani wa maisha yao. Askofu awe daima ni kiongozi anayewasha moto na mwanga wa matumaini kwa waamini wake, akiongozwa na uvumilivu wa Mungu katika kuwaongoza watu wake.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Askofu anapaswa kuwa kati ya watu wake katika mambo makuu matatu: daima awe mstari wa mbele, ili kuwaonesha dira na njia ya kufuata ili wasitangetange na kuyumbishwa kiasi hata cha kutokomea porini. Askofu awe nyuma ya waamini wake, ili kuhakikisha kwamba, hakuna aliyeachwa wala kusahaulika, lakini zaidi, waamini wenyewe kama sehemu ya mchakato wa ukomavu wanaweza kujiongoza wenyewe bila ya kuwa na lazima ya kufuatwa fuatwa hata kwa mambo ya kawaida.

Baba Mtakatifu anahitimisha hotuba yake kwa Sekretarieti ya Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini na Caribbean kwa kuwaambia kwamba, kwa sasa shughuli za kichungaji zinatindikiwa na wongofu wa ndani, changamoto kwa viongozi wa Kanisa na waamini katika ujumla wao, kusaidiana kuanza tena kwa moyo mkuu, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa Amerika ya Kusini.

Imehaririwa na Padre Richard Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.