Dumisheni amani na utulivu wakati mkisubiri matokeo rasmi ya uchaguzi mkuu
Tume ya haki na amani ya Shikirisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Kusini mwa Afrika,
IMBISA, inawataka waamini na wananchi wa Zimbabwe katika ujumla wao kuhakikisha kwamba,
wanaendeleza amani na utulivu, wakati huu wanaposubiri Tume ya Uchaguzi Zimbabwe kutangaza
matokeo rasmi ya uchaguzi mkuu uliofanyika hivi karibuni.
IMBISA inaishauri
Tume ya Uchaguzi Zimbabwe kujitahidi kutangaza matokeo ya uchaguzi mkuu, kadiri ya
taratibu na sheria za nchi. Hadi sasa IMBISA imeridhika na mchakato mzima wa uchaguzi
mkuu nchini Zimbabwe kwa Mwaka 2013. Amani na utulivu vimetawala maeneo mengi, ikilinganishwa
na chaguzi zilizopita. Wananchi waliendelea kuonesha utulivu hata pale vituo vya kupigia
kura vilipochelewa kufunguliwa kadiri ya ratiba.
Katika uchaguzi mkuu, kuna
kasoro ndogo ndogo ambazo zimejitokeza, hii ni pamoja na baadhi ya wananchi kutoona
majina yao kwenye Daftari la wapiga kura, ingawa wanadai kwamba, walijiandikisha.
Kuna baadhi ya wananchi hawakufanikiwa kupiga kura hata kama walikuwa wamejiandikisha.
Ni kasoro ndogo ndogo zilizojitokeza kwenye uchaguzi mkuu nchini Zimbabwe, lakini
mambo yamekuwa ni shwari, dalili za ukomavu wa kisiasa na changamoto ya kukumbatia
demokrasia ya kweli.
Wakati huo huo, Bwana Bernard Membe, Waziri wa mambo
ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa kutoka Tanzania ambaye ni mtamzaji kutoka
SADC, akizungumza na waandishi wa habari, mwishoni mwa juma, amesema kwamba, uchaguzi
mkuu nchini Zimbawe ulikuwa huru na amani. Anawataka wanasiasa nchini Zimbabwe kukubali
matokeo rasmi yatakayotangazwa na Tume ya uchaguzi nchini Zimbabwe.