Waandishi wa habari Wakatoliki wanachangamotishwa kuwa ni mashahidi wa Kristo Mfufuka!
Njia za mawasiliano ya jamii ni nyanja inayokabiliana na mabadiliko makubwa katika
ulimwengu wa sayansi, teknolojia na kitamaduni hata katika maisha, utume na historia
ya Kanisa.
Ni mchango wa Askofu mkuu Claudio Maria Celli, Rais wa Baraza la
Kipapa la Mawasiliano ya Jamii katika hotuba yake ya ufunguzi wa Mkutano mkuu wa Waandishi
wa habari Wakatoliki kutoka Amerika ya Kusini,(OCCLAC) uliofunguliwa hapo tarehe Mosi,
Agosti na unafungwa, Jumamosi, tarehe 3 Agosti 2013.
Akizungumzia mikakati
ya mawasiliano kwa mwaka 2013 hadi mwaka 2017, alisema kwamba, waandishi wa habari
wanapaswa kuwa ni vyombo vya ujenzi wa utamaduni wa kukutana na watu, ili kubomoa
vikwazo na vizingiti vinavyojitokeza katika ulimwengu wa mawasiliano ya jamii, kiasi
kwamba, watu wanashindwa kuwasiliana barabara hata kama wako kwenye mitandao ya kijamii.
Watu washirikiane kwa dhati ili kutokomeza upweke hasi unaoendelea kusababisha
madhara makubwa katika maisha, ustawi na maendeleo ya watu. Ikumbukwe kwamba, mwanadamu
ndiye anayepaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika mawasiliano na wala si vyombo
vya mawasiliano. Watu wajifunze kukutana na kuwasiliana ili wajenge umoja na mshikamano.
Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuwachangamotisha waandishi wa habari
kushirikisha utajiri wa imani yao kutoka kwa Kristo na Kanisa lake, lakini baada ya
kukutana na Yesu katika: Maandiko Matakatifu, Sakramenti za Kanisa na kwa watu wanaosukumizwa
pembezoni mwa Jamii. Bado kuna vikwazo vinavyoikabili sekta ya mawasiliano ya kijamii
sehemu mbali mbali za dunia kwani kuna watu wanaendelea kupigania uhuru wa kujieleza
na uhuru wa vyombo vya habari.
Vyombo vya habari vinavyomilikiwa na kuendeshwa
na Kanisa vinapaswa kuwa mstari wa mbele kusimama kidete kulinda na kutetea ukweli,
utu na heshima ya binadamu; haki msingi za binadamu mintarafu kweli za Kiinjili, maadili
na utu wema. Vyombo hivi anasema, Askofu mkuu Claudio Maria Celli, vinapaswa kuwatangazia
watu wanaoishi pembezoni mwa jamii, Habari Njema ya Wokovu, kwa kutambua kwamba, Uinjilishaji
unamgusa mtu mzima: kiroho na kimwili, ili kuiona na kuitambua ile sura na mfano wa
Mungu katika maisha ya kila mwanadamu.
Waandishi wa habari Wakristo wasukumwe
kutangaza tunu msingi za maisha ya kiutu, kimaadili mintarafu Mafundisho na Kweli
za Kiinjili, daima wakiongozwa na dhamiri nyofu. Wawe ni watu wanaofanya tafakari
ya kina, ili kuendelea kutafuta utekelezaji wa mapenzi ya Mungu katika maisha na taaluma
yao kama waandishi habari Wakatoliki.
Ni matumaini ya Askofu mkuu Claudio
Maria Celli kwamba, waandishi habari Wakatoliki kutoka Amerika ya Kusini, watakuwa
ni mashahidi bora wa Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu!