2013-08-02 08:17:33

Mwenyeheri Yohane XIII na Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican


Maisha ya Mwenyeheri Yohane wa XXIII yalijikita zaidi katika maisha ya kawaida na busara, kielelezo cha hali ya juu cha falsafa ya mwanadamu. Hii ndiyo iliyokuwa dira na mwongozo wa maisha ya Mwenyeheri Papa Yohane wa XXIII. RealAudioMP3

Familia ya Mungu inafurahia tamko la kwamba, Mama Kanisa anatarajia kuwatangaza Mwenyeheri Yohane wa XXIII na Yohane Paulo II kuwa watakatifu, wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Jubilee ya Miaka 50 ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican sanjari na Mwaka wa Imani.

Papa Roncali ni kiongozi ambaye hakuwa na wasi wasi katika hija ya maisha ya imani, daima alionesha amani na utulivu wa ndani. Akiwa Padre kijana kabisa aliwahi kusema kwamba, amana kubwa ambayo anaihifadhi katika undani wa moyo wake ni IMANI, aliyorithi kutoka kwa wazazi wake! Hii ndiyo imani ambayo alisimama kidete kuilinda na kuwamegea wengine katika maisha yake kama Padre, Askofu na Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Ni imani iliyomuunganisha na Kristo pamoja na Kanisa lake, kiasi cha kumsukuma kuwashirikisha wengine, tangu alipokuwa mtumishi wa Altareni Parokiani mwake, mchakato ambao ameuendeleza kwa ari na moyo mkuu kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Hii ndiyo imani iliyomsukuma kuwa na ujasiri wa kutangaza na hatimaye, kuadhimisha Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, hapo tarehe 11 Oktoba 1962. Hapa Familia ya Mungu ikasimama na kuungama Imani kwa Kanisa moja, takatifu, katoliki na la mitume!

Huu ni urithi mkubwa ambao Papa Yohane wa XXIII ameliachia Kanisa la Kristo. Hii ndiyo imani inayowaimarisha waamini hata kujitosa kimaso maso kupambana na changamoto za maisha kwa ujasiri na umakini mkubwa! Alisikika daima akisema kwamba, mtu mwenye imani thabiti kamwe hawezi kutetereka!Nabii Isaya anasema, kwa ajili ya hayo Bwana, Mungu, asema hivi, ”Tazama, naweka jiwe katika Sayuni, liwe msingi, jiwe linalojaribiwa, jiwe la pembeni lenye thamani, msingi ulio imara: yeye aaminiye hatafanya haraka. Isaya 28: 16 .

Papa Yohane wa XXIII alikuwa ni kiongozi mwenye unyenyekevu mkubwa, fadhila ambayo iliongoza maisha na huduma yake kwa Kanisa kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ni kumbu kumbu endelevu ya unyenyekevu na huduma makini iliyotolewa na Papa Yohane wa XXIII katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kanisa linasubiri kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani.

Hivi ndivyo Monsinyo Loris Capovilla anavyochambua utakatifu wa maisha ya Mwenyeheri Yohane wa XXIII.

Imehaririwa na Padre Richard Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.