Mradi wa kuwawezesha wasichana wasanii, Kenya waanza kutimua vumbi!
Mshiriki mmoja mashuhuri wa mashindano ya “Tusker Project Fame” yenye kuwahusisha
wasanii chipukizi, Bi. Amileena Mwenesi sasa ameanzisha mradi wa kuwasaidia wanamuziki
chipukizi wa kike nchini Kenya kutambua na kukuza vipaji vyao.
Mradi huo unaojulikana
kama “Mafao ya Msichana” umewapatia nafasi wasichana sita kujiunga na mafunzo ya dhati
ya majuma sita ambapo wanasaidiwa kunoa vipaji vyao vya uimbaji kama matayarisho kwa
ajili ya kushiriki kwenye hafla ya wasanii itakayofanyika mnamo Agosti 17, 2013.
Lengo
la mradi wa Mafaa ya Msichana ni kusaidia kunoa na kukuza vipaji vya wasanii wa kike
walio na msimamo wa maadili. Wasichana sita ambao wamebahatika kuwa wa kwanza kufaidi
mafunzo yaliyoandaliwa na mradi wa Mafao ya Msichana ni miongoni mwa wasichana walioweza
kufikia fainali katika mchuano wa majaribio ya sauti yaliyoandaliwa na kampuni ya
Liberate Agency, ambayo pia huwaunda wasichana wasanii ili waweze kufaulu kwenye malengo
yao maishani, na hushirikiana na jitihada kama zile za Mafao ya Msichana ili kuwajengea
vipaji wasanii chipukizi.
Mwanzilishi wa Mafao ya Msichana, Amileena Mwenesi
anasema kwamba, Liberate Agency ni kampuni ya Sanaa inayowapa fursa wasanii chipukizi
kuboresha picha na sauti zao katika harakati za kujijenga kisanii. Mradi huu umeteuliwa
na kampuni ya Liberate Agency kwa mwaka 2013 katika juhudi za huduma kwa jamii inaonyesha
jitihada za kampuni hiyo katika kuwaunda wasichana ili waweze Kujifunza, kufikiri,
kujieleza, kuhusiana na wengine, na kujiheshimu vilivyo katika mambo yanayohusu taaluma,
na hivyo kuyamudu maisha yao vyema.