UNICEF: Watoto milioni 223 wanaathirika kutokana na nyanyaso na dhuluma
Uonevu na nyanyaso dhidi ya watoto ni visa vinavyoyaepuka macho na masikio ya watu
wengi kwani mara nyingi havifikishwi kwenye vyombo vya sheria. Haya yamesemwa na
Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa, (UNICEF). Shirika hili limewaomba
watu binafsi, wanasheria, na serikali za nchi mbali mbali kutofumbia macho vitendo
vya unyanyasaji wa watoto duniani.
Shirika hili linapinga visa vya kinyama
na uonevu dhidi ya watoto vinavyozidi kujitokeza kama kile kisa cha kupigwa risasi
mtotoMalala Yousafazai huko Pakistani, na kile kisa cha kuwaua kwa risasi watoto 26
na walimu wao kwenye shule moja ya Newton, Connecticut, nchini Marekani mnamo mwezi
Desemba, 2012. Matukio mengine ni ya unyanyasaji wa wasichana nchini India na Afrika
ya Kusini kwa mwaka 2013.
Mateso dhidi ya watoto ni jambo linaloikabili kila
nchi na tamaduni, anasema Mkurugenzi wa UNICEF, Anthony Lake, na kwamba kila mara
mtoto yeyote anapokumbwa na mateso mahali popote duniani, watu hawana budi kuonyesha
masikitiko yao na kusaidia kuyaleta hadharani mateso haya mengi yakiwa yanatendeka
kisiri.
Huu ni ujumbe wa kwanza kwenye kampeni ya UNICEF ya kutaka kusitisha
unyanyasaji dhidi ya watoto. Kampeni hii ya kimataifa inawalenga watu wote duniani
ili waweze kutambua na kuondokana na visa vya unyanyasaji dhidi ya watoto, ili kujenga
utamaduni wa kuwahehimu, kuwathamini na kuwalinda watoto katika malezi na ukuaji wao.
Uzinduzi
wa kampeni hii umefanyika kupitia video ambapo Balozi wa Matashi Mema wa UNICEF, Liam
Neeson anasikika akiwaongoza watazamaji kuona visa mbalimbali vya unyanyasaji vinavyowakabili
watoto kisirisiri. Mfano wa visa hivyo ni pamoja na kile cha ubakaji wa msichana wa
miaka 15 mikononi mwa kundi la vibaka; na mtoto anayepigwa hadi kuumizwa vibaya na
mwalimu wake kwa kukosa kujibu swali kwa usahihi baada ya kuulizwa na mwalimu wake
darasani.
Balozi huyu wa matashi Mema wa UNICEF, Liam Neeson anasema kwamba,
kwa vile visa vingi havitendeki hadharani, haimaanishi kwamba havitokei, na anawashawishi
watu wote wa mapenzi mema kushiriki katika kampeni hii, ili kuweza kuviweka hadharani
visa vyote vinavyotendeka dhidi ya watoto, hata kama vinatendeka katika uficho mkubwa.
Kulingana
na taarifa ya Shirika la Afya Duniani ya Mwaka 2005, zaidi ya watoto milioni 150 wa
kike na watoto wengine milioni 73 wa kiume chini ya miaka 18 wamepitia madhulumu na
nyanyaso za kijinsia, na kwamba, watoto wengine milioni 1.2 kila mwaka huangukia kwenye
soko la biashara haramu ya binadamu.
Inapaswa kukumbukwa kwamba, visa hivi
haviachi majeraha mwilini mwa watoto waathirika, bali pia kwenye akili na utu wao
kwa ujumla na kwamba, vinaathiri pia uwezo wao wa kuelewa, kukua na kuchangamana na
wenzao katika jamii.
Kuwatetea na kuwalinda watoto duniani ni lengo na kiini
cha majukumu ya UNICEF. Tamko la Haki za Watoto la Umoja wa Mataifa linafafanua kwamba,
kila mtoto, popote pale alipo, ana haki ya kulindwa dhidi ya uonevu na mateso ya aina
yoyote ile.