2013-07-31 10:32:43

Watu wasiomwogopa Mungu na kumthamini binadamu, vita itakoma duniani!


Wananchi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, hapo tarehe 12 Agosti 2013 wataungana kusali kwa ajili ya kuombea amani na utulivu nchini mwao, kama sehemu ya mkesha wa kumbu kumbu ya Uhuru nchini humo.

Viongozi wakuu wa dini nchini humo katika kikao chao cha tarehe 19 Julai 2013 wameamua kwa kauli moja kuwaunganisha waamini wa dini na madhehebu mbali mbali kuunganika kwa pamoja kwa ajili ya kusali ili kuombea amani kwani hakuna dini yoyote duniani inayotangaza na kushabikia vitendo vya mauaji ya kinyama, wizi, uporaji na nyanyaso dhidi ya wanawake na wasichana.

Viongozi wa kidini wanawataka wanasiasa kujikita katika misingi ya maadili, ukweli na uwazi, uaminifu, sheria na kanuni zinazoongoza nchi, kwa kuwaheshimu na kuwalinda wananchi wote wa Afrika ya Kati bila ya kuwa na upendeleo wa kidini, kisiasa, kikabila au kijinsia. Serikali inawajibu wa kuwalipa wafanyakazi wake mishahara yao wanapotekeleza majukumu yao kadiri ya sheria za nchi.

Viongozi wa kidini na madhehebu mbali mbali nchini Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati wanawataka wanajeshi wa Seleka kutubu na kuongoka ili kuachana na vitendo vya mauaji ya watu wasiokuwa na hatia; wawe na ujasiri wa kulinda na kutetea maisha ya watu, kwani hao wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Hata wanajeshi wa Seleka wanapaswa kuongozwa na maadili na utu wema badala ya kuendeleza vitendo vya kihuni nchini humo. Ni mwaliko kwa vijana kukataa katu katu kutumiwa kwa ajili ya masilahi na mafao ya watu wachache nchini Afrika ya Kati kwa kumwogopa Mwenyezi Mungu kwanza kabla ya mambo mengine yote.







All the contents on this site are copyrighted ©.