Utunzaji bora wa mazingira na maendeleo endelevu ni kati ya mambo yanayopewa kipaumbele
na Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani
Uhusiano kati ya mazingira na maendeleo endelevu kati ya binadamu wote umepewa kipaumbele
cha pekee kwenye barua ya hivi karibuni iliyoandikwa na Baraza la Maaskofu Katoliki
Marekani. Barua hiyo, iliyowekwa sahihi na maaskofu Stephen Edward Blare, Rais
wa Tume ya Kitaifa ya Haki na Maendeleo ya Watu na Richard Edmund Pates wa Tume ya
Haki na Amani Kimataifa, imetumwa kwa mjumbe wa Uchumi wa Serikali ya Marekani, Balozi
Michael Froman na inaashiria kwamba, katika nyanja za biashara, kuna uhitaji wa maadili
yanayotokana na kuheshimu utu na hadhi ya binadamu. Barua hiyo pia inasema kwamba,
faida na lengo la ushirikiano wa kiuchumi vinapaswa kuwa ni uboreshaji wa maisha hasa
ya wafanyakazi maskini, wanyonge pamoja na familia zao. Baraza la Maaskofu Katoliki
Marekani pia linasema kwamba, kuna uhitaji wa kulinda na kudumisha hadhi na heshima
ya binadamu kwa kuzingatia sio tu haki za kikazi, bali pia haki za watu mahalia, kushughulikia
vyanzo vya tatizo la uhamiaji, kuendeleza watu wanaoishi vijijini pamoja na kutunza
mazingira, kazi ya uumbaji ambayo Mwenyezi Mungu amemkabidhi mwanadamu. Pia makubaliano
yoyote ya kiuchumi na kibiashara ni lazima yasaidie kupunguza deni la nje linalozikabili
nchi maskini duniani, pamoja na kuzisaidia nchi hizo kukua na kushiriki kikamilifu
kwenye maamuzi ya kiuchumi na kibiashara katika medani za kimataifa.