2013-07-31 15:56:34

"Mkitumbukiza udini katika siasa, mtasababisha maafa makubwa Tanzania"!


Rais Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania amesema kuwa kasi ya kuingia kwa wahamiaji haramu katika Mkoa wa Kagera inatisha na kuwa kwa kiasi kikubwa baadhi ya Idara za Serikali na hasa Uhamiaji zinahusika na kasi hiyo. Aidha, Rais kikwete amesema kuwa Tanzania itaendelea kukaribisha watu wanaotaka kuingia nchini, na hata kuomba uraia kutoka nje, lakini watu hao lazima wafuate Sheria za Uhamiaji za nchi hii.

Rais pia amesema kuwa Tanzania haiwezi kufanywa sehemu ya watu kuingiza mifugo yao kwa ajili ya malisho tu, ama kuruhusu watu waliopewa nafasi ya kuwa raia wa nchi hii lakini wakakataa kuomba uraia, kuendelea kuishi nchini kinyume cha Sheria. Rais Kikwete alikuwa anazungumza na viongozi wa Mkoa wa Kagera, Jumatatu, Julai 29, 2013, wakati anafanya majumuisho ya ziara yake ya siku sita Mkoani humo kwenye Ikulu Ndogo mjini Bukoba.

Mkoa wa Kagera ambao unapakana na nchi tatu za Burundi, Rwanda na Uganda, unakadiriwa kuwa na wakimbizi haramu wapatao 52,000 na idadi hiyo inaendelea kuongezea siku hata siku. Rais Kikwete amewaambia viongozi hao kuchukua hatua za haraka kupambana na kasi hiyo mbali na operesheni maalum ya Majeshi ya Ulinzi na Usalama ambayo inatakiwa kuendeshwa karibuni kusakama majambazi na wahamiaji haramu katika mikoa ya Kagera, Kigoma na Geita kama alivyoelekeza majuzi Rais Kikwete ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu.

“Tutafanya operesheni hii kubwa, lakini jibu la kudumu siyo operesheni na wala tusingelazimika kufanya operesheni hii kama Idara za Serikali hasa Uhamiaji zingefanya kazi yake kwa umakini unaostahili, na kama watendaji wa Serikali katika vijiji, kata na tarafa wangefanya kazi yao vizuri bila kuhongwa. Wahamiaji haramu wanaingia nchini kwa urahisi kwa sababu wamejua thamani na bei yenu – ambayo ni ya chini sana.”

“Tumefikia hapa kwa sababu ya udhaifu wa Idara ya Uhamiaji na watendaji wa kata na vijiji kujifanya maofisa uhamiaji. Nani kawapa kazi hii kama siyo kuhongwa ngo’mbe wawili watatu? Kisingizio hatuna usafiri mbona hapa Bukoba mjini wapo? Mbona Kayanga wapo? Mbona Ngara mjini wapo?”

Ameongeza Rais Kikwete: “Kuna mtu pale mpakani, anajulikana kwa jina, kazi yake ni kuingiza wahamiaji haramu katika Tanzania. Hakamatwi kwa nini? Kwa sababu pamoja na mambo mengi anapokea rushwa? Sijawahi mimi kuona mtu anapokea rushwa hadharani, anajulikana kwa jina, wanaompa rushwa wanajulikana na akaendelea kuwa huru? Huu ni upungufu mkubwa wa mfumo wa utawala bora. Uhamiaji timizeni wajibu wenu ili watu wajue Serikali ipo.”

Amesema kuwa mwenendo huu wa baadhi ya Idara za Serikali ni hatari. “Mnatengeneza tatizo kubwa sana kwa sababu katika miaka 50 ijayo muundo wa wakazi wa mkoa huu utabadilika sana. Hili ni jambo kubwa na tunalifanya ovyo ovyo. Mnafanya mchezo wa hatari na jambo hili kubwa. Kasi ya kuhamia bila kufuatia sheria imekuwa kubwa sana.”

“Sisi hatuwazuii watu kuja Tanzania na kuishi, lakini anayetaka kuja Tanzania afuate sheria na taratibu zetu za uhamiaji. Wengine tuliwapa nafasi ya kuwa raia, wakakataa. Hawa warudi makwao na wanaotaka kurudi makwao tutawasaidia kurudi makwao. Wengine wanakuja kuchunga mifugo yao, hata kama Tanzania ina malisho mazuri lakini ni nchi tofauti na zile wanakotoka lazima waingia nchini kisheria.”

Amesema kuwa Tanzania ina historia ya kututuka sana ya kukaribisha wageni na wakimbizi na hata kuwapa uraia. “ Mwaka 1982, Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere alitoa uraia wa wakimbizi 30,000, mimi nimetoa uraia wa wakimbizi 160,000? Nchi gani inafanya hivyo kwa kiasi kikubwa namna hiyo? Hivyo, dhamira yetu katika kukaribisha wageni haiwezi kutiliwa shaka na yoyote. Tunachoomba sisi ni watu waingie nchini kwa kufuata taratibu na sheria tu.”

Kuhusu zoezi la kuwaondoa wahamiaji haramu, Rais Kikwete ameelekeza kuwa waondolewe bila kubughubiwa kama hawakatai kuondoka. “Msiwabughudhi, msiwanyang’anye mali zao, Kama mtu ana biashara zake mpe muda wa kuziuza na baada ya hapo aondoke. Lakini lazima aondoke.”


Rais kikwete: Nitaendelea kulikemea suala la udini hata kama baadhi wanachukia

Rais Kikwete ameonya kuwa ushabiki wa baadhi ya viongozi wa dini kuingiza udini katika siasa na hasa kama jambo hilo litakubaliwa kuwa sehemu ya uendeshaji siasa za Tanzania, basi huo ndio utakuwa mwisho wa utulivu wa Tanzania. Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa hata kama baadhi ya viongozi wa dini wanamchukia kwa kulisemea jambo hilo hadharani, ataendelea kulisemea hadharani, bila woga wala kificho, kwa sababu “kuitumbukiza dini katika siasa ni kuipeleka nchi mahali sipo.”

Rais Kikwete pia amesema kuwa ni jambo la hatari kwa baadhi ya Watanzania ambao ni viongozi kushabikia jambo hilo kwa sababu mivutano na ugomvi wa kidini siyo ajenda ya Tanzania na kwa baadhi ya viongozi wa dini zote kujitumbukiza katika suala hilo ni kucheza ngoma isiyo ya nchi ya Tanzania.

Rais Kikwete ametoa onyo hilo wakati alipozungumza na viongozi wa Mkoa wa Kagera wakati wa majumuisho ya ziara yake ya siku sita mkoani humo Ikulu Ndogo mjini Bukoba. Katika majumuisho hayo ambako Rais Kikwete amezungumzia mambo mengi amesisitiza: “Wako watu wanaosaka kuvuruga amani ya nchi yetu kwa udi na uvumba na baadhi yetu tumetumbukia katika hilo kwa kupitia udini na siasa. Na inashangaza kuona kuna mivutano ya kidini nchini kwa sababu hakuna kitabu kipya cha dini kilichotolewa na dini yoyote hapa nchini. Vita Vitakatifu ni vile vile, lakini bado mwelekeo wa dini katika nchi yetu umebadilika, mahubiri ya msingi ni yale yale.”

Ameongeza Rais Kikwete: “Ukweli ni kwamba ajenda ya udini siyo ajenda ya Watanzania, siyo ajenda yetu, hata kama baadhi yetu wanashabikia kupitia siasa ambayo ni hatari kweli kweli. Ndugu zangu nawashaurini tusicheze ngoma isiyo yetu, unyago huu siyo wetu sisi.”

Rais amesema kuwa anajua kuwa wapo watu wanaomchukia anapolisemea jambo hilo lakini akaongeza: “Nichukieni tu lakini nitaendelea kulisemea hili. Wanachukua udini na kuutumbikiza katika siasa na likizama huko halitoki tena. Linalofuata ni kutengeneza siasa za watu wa dini yako, kuchaguliwa kwa dini yako na siyo kwa sifa na uwezo. Na jambo hili siku likiingia kweli kwenye katika siasa huo ndio utakuwa mwisho wa utulivu wa nchi hii.”

“Ni jambo halina maana, halina faida wala busara yoyote. Litawagawa wananchi wetu kwa misingi ya dini. Na ishangaza kwamba wapo viongozi wa dini zote mbili wanalishabikia hili – jambo litakalofuata ni kutugawa na kuigawa nchi hii – nusu Wakristo, nusu Waislamu.”

Rais amepongeza ushirikiano wa viongozi wa dini kuu katika Mkoa wa Kagera akisisitiza kuwa uhusiano huo ni muhimu na unafaa kuendelezwa na kuwekewa misingi imara zaidi.









All the contents on this site are copyrighted ©.