Miamba wawili wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kutangazwa watakatifu!
Baba Mtakatifu Francisko baada ya kusikiliza na maoni ya Makardinali na Maaskofu wakuu
ameamua kuitisha mkutano wa Makardinali utakaoridhia Kanisa kuwatangaza Papa Yohane
wa Ishirini na tatu na Yohane Paulo wa Pili kuwa Watakatifu.
Hayo yamesemwa
na Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa
wenyeheri na watakatifu, mara baada ya kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko
hivi karibuni.
Baba Mtakatifu ameridhia kuchapishwa kwa hati zinazotambua
miujiza iliyotendwa na Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili, miaka michache tu, tangu alipotangazwa
kuwa ni Mwenyeheri. Mama Kanisa anapoadhimisha Jubilee ya Miaka 50 ya Mtaguso Mkuu
wa Pili wa Vatican sanjari na Mwaka wa Imani, anapenda kuwaweka Papa Yohane wa XXIII
pamoja na Mwenyeheri Yohane Paulo II kuwa ni mifano hai ya kuigwa katika maisha na
utume wa Kanisa.
Haya ni matunda ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, tukio
la: Kiekuemene; Upendo na Amani ya Kiinjili; kielelezo makini cha Mama Kanisa anayemjali
mwanadamu katika maisha yake yote; wakati wa raha na machungu, daima anapania kumkirimia
imani, matumaini na mapendo. Mwenyeheri Yohane wa XXII alitambulikana kuwa ni Papa
mwema, Baba wa Wakatoliki na wasioamini, aliwakumbatia wote na kuwabariki.
Mwenyeheri
Yohane Paulo wa pili, katika hija zake za kichungaji sehemu mbali mbali za dunia,
ametangaza kwa maisha na maneno yake Injili ya Upendo, Haki na Amani; amekuwa ni kielelezo
cha udugu, umoja na mshikamano kati ya watu wa mataifa; kwa kuonesha ukarimu kwa maskini
na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.
Kardinali Angelo Amato anasema,
viongozi hawa wawili ni wadau wakuu wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, kwa pamoja
wameonesha fadhila ya utakatifu wa maisha ya Kikristo mintarafu utume na mazingira
waliyokutana nayo katika nyakati zao. Yohane XXIII alionesha ujasiri mkubwa kwa kuitisha
Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican na matunda ya Mtaguso huu yanaendelea kujionesha katika
maisha na utume wa Kanisa.
Mwenyeheri Yohane Paulo wa II akamwilisha Mafundisho
ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kwa kushirikisha karama na fadhila ambazo alikuwa
amekirimiwa na Mwenyezi Mungu katika maisha yake: akakazia taalimungu, sheria za Kanisa
na Katekesi. Yohane wa XXIII alianzisha mchakato wa mabadiliko ndani ya Kanisa, akayaita
“Aggiornamento”, Yohane Paulo II akatekeleza kwa uaminifu mkubwa mawazo
ya Mababa wa Mtagauso Mkuu wa Pili wa Vatican.
Viongozi hawa wawili wametekeleza
dhamana yao kama Makhalifa wa Mtakatifu Petro kwa umakini mkubwa, wote wakiwa na Ibada
ya pekee kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Bikira Maria akawa ni kielelezo
cha imani na ufuasi wa Kristo.
Kardinali Angelo Amato anasema, bila shaka
wengi wanakumbuka lile tukio la ajabu lililotokea tarehe 13 Mei 1981, alipopigwa risasi
kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, lakini akasalimika baada
ya mateso na mahangaiko makubwa; tangu wakati huo, akatambua na kuuona ulinzi wa Bikira
Maria katika maisha na utume wake!
Vijana waliokuwa wamekusanyika kwenye Uwanja
wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, wakati walipokuwa wanamsindikiza Baba
Mtakatifu Yohane Paulo wa pili katika dakika zake za mwisho mwisho kabla ya kuitupa
mkono dunia, waliposikia kwamba, amefariki, wakapiga kelele na kuandika, “Santo Subito”,
atangazwe mara moja kuwa mtakatifu! Ni ushuhuda uliotolewa na watu hata kabla ya kuanza
mchakato wa kumtangaza kuwa ni Mwenyeheri.
Kardinali Angelo Amato anasema
kwamba, Kanisa limefuata hatua kwa hatua mchakato mzima wa kumtangaza Yohane Paulo
wa pili kuwa Mwenyeheri, bila kuwa na haraka wala shikinikizo lolote! Kanisa linapenda
kufanya mambo yake kwa busara na hekima!
Mama Kanisa katika kipindi cha Miaka
ya hivi karibuni amebahatika kuwa na Kundi kubwa na Watakatifu, ambao wamekuwa ni
viongozi wakuu wa Kanisa. Ni Mapapa walionesha hekina na utakatifu wa maisha. Hawa
ni Pio XII; Yohane XXIII; Yohane I; Yohane Paulo II. Ni viongozi walionesha utakatifu
wa maisha katika utume wao kama Makhalifa wa Mtakatifu Petro.
Kutokana na
maisha yao ya utakatifu, bado wanakumbukwa, wanapendwa na kuthaminiwa na wengi. Kanisa
bado linaendelea kuiangazia dunia kwa mwanga wa utakatifu wa wachungaji wake wakuu!
Imehaririwa
na Padre Richard Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.