Dodoma washerehekea miaka 10 ya Shule ya Awali ya Mtakatifu Inyasi wa Loyola
Shule ya Msingi ya Mtakatifu Inyasi wa Loyola, iliyoko Jimbo Katoliki la Dodoma inayoendeshwa
na Wayesuit, inasherehekea miaka kumi tangu ilipoanzishwa ili kutoa nafasi hata kwa
watoto wa wakulima Jimboni Dodoma kupata elimu bora itakayowasaidia kupambana na mazingira
yao kwa sasa na kwa siku za usoni.
Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi
na sita, katika Waraka wake wa kichungaji, Dhamana ya Afrika anabainisha kwamba, shule
zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki Barani Afrika ni rasilimali ya thamani
kwa majiundo ya watu tangu wakiwa watoto, ili kujenga na kudumisha mshikamano wa umoja,
haki na amani. Ni mahali ambapo watoto wanafundishwa tunu msingi za kiutu na maisha
ya Kiinjili, changamoto kwa Kanisa Barani Afrika kuwekeza zaidi katika sekta ya elimu
kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Bara la Afrika.
Elimu ijikite katika ukweli
wa maisha unaopania kujenga misingi ya haki, amani na upatanisho wa kweli pamoja na
kuwasaidia watoto na vijana wa Bara la Afrika kutambua fursa na changamoto zilizoko
mbele yao katika ujenzi wa nchi na Bara la Afrika kwa ujumla.
Katika mahubiri
ya Misa ya shukrani kwa ajili ya Maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Miaka 10 tangu Shule
ya Msingi ya Mtakatifu Inyasi wa Loyola, Jimbo Katoliki la Dodoma ilipofunguliwa rasmi
na Askofu mstaafu Mathias Isuja Josefu, Padre Chesco Peter Msaga, Makamu Askofu Jimbo
Katoliki Dodoma, amewataka waamini kujenga moyo na utamaduni wa shukrani kwa Mwenyezi
Mungu kutokana na mapaji na zawadi mbali mbali anazowakirimia katika maisha.
Waamini
watambue kwamba, mafanikio, mali, fedha na yote waliyo nayo wamejaliwa na Mwenyezi
Mungu na wala si kwa bahati nasibu au kutokana na ujanja wao. Hivyo wanapaswa kujifunza
kuwashirikisha na kuwamegea wengine utajiri kwa njia ya mshikamano katika matendo
ya huruma na mafao ya wengi. Kwa njia hii wanaweza kuonesha moyo wa shukrani unaojikita
katika mshikamano wa upendo.
Katika sherehe hizi, Dr. Rehema Nchimbi, Mkuu
wa Mkoa wa Dodoma, alitumia fursa hii kuwaalika wadau mbali mbali wanaotaka kuwekeza
katika sekta ya elimu mkoani Dodoma kujitokeza kwani kwa sasa Dodoma ina mvuto mkubwa
na inaendelea kujitanua katika medani mbali mbali za maisha. Lengo la Tanzania ni
kuhakikisha kwamba, watanzania wanapata msingi wa elimu bora itakayowasaidia kupambana
na mazingira yao kikamilifu.
Dr. Rehema amewataka wazazi kuhakikisha kwamba,
wanachangia kikamilifu katika huduma za elimu kwa watoto wao, kwani huu ndio urithi
bora zaidi, sanjari na kuhakikisha kwamba, wanafuatilia ufanisi wa majiundo ya watoto
wao: kitaaluma, kitu na kiroho. Wazazi wamehimizwa kushirikiana na walezi pamoja na
walimu kwa ajili ya malezi ya watoto wao katika sekta mbali mbali za maisha.
Naye
Sr. Euphrasia Mwingira, Mkuu wa Shule ya Awali ya Mtakatifu Inyasi amesema, pamoja
na mambo mengine, shule yao inakabiliwa na barabara dunia zinazoingia katika eneo
la "Swaswa kwa Wasomi".