Boko Haram bado inaendelea kusababisha maafa nchini Nigeria
Kikundi cha Kigaidi cha Boko Haram, tarehe 29 Julai 2013 kimefanya shambulizi kwenye
Kitongoji cha Sabon Gari na kusababisha vifo vya watu 12, licha ya kampeni kubwa inayoendeshwa
na Serikali kutaka kukidhibiti Kikundi cha Boko Haram katika maeneo ya Kaskazini mwa
Nigeria.
Taarifa ya vyombo vya habari kutoka Nigeria inabainisha kwamba, watu
40 wanaotuhumiwa kuhusika na shambulizi hili tayari wamekwishakamatwa. Wananchi wametakiwa
kuchukua tahadhari kubwa kwani wanaweza kushambuliwa wakati wowote.
Katika
mahojiano na Radio Vatican, Kardinali John Onayekan wa Jimbo kuu la Abuja, Nigeria
anasema, inasikitisha na kutia uchungu kuona watu wasiokuwa na hatia wanaendelea kupoteza
maisha yao kwa vitendo vya kigaidi nchini Nigeria. Hii inaonesha kwamba, amani haiwezi
kupatikana kwa kutunishiana misuli kati ya Serikali na Kikundi cha Boko Haram, ambacho
kimekuwa kikihusika na mashambulizi ya kigaidi nchini Nigeria.
Kuna haja ya
kuendeleza majadiliano ya kidini ili kuweka mikakati ya ujenzi wa Nigeria mpya inayojikita
katika misingi ya haki, amani, utulivu na maendeleo endelevu. Pengine tatizo la kikundi
cha Boko Haram halijapewa kipaumbele cha kutosha, ndiyo maana kinaendelea kusababisha
maafa makubwa kwa watu na mali zao. Serikali inapaswa kuendeleza mikakati ya ulinzi
na usalama kwa ajili ya wanananchi wa Nigeria.
Kardinali Onayekan anasema
kuna umuhimu pia kwa wananchi wengi nchini Nigeria kuhusishwa katika mchakato wa kulinda
na kudumisha misingi ya haki, amani na utulivu, kwani bila amani na utulivu mambo
mengi yataendelea kuharibika nchini Nigeria.