Katika shida na mahangaiko ya watu kutokana na vita pamoja na kukosa makazi, kuna
haja kwa Jamii kuheshimu utu wa wanawake wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwani
wanaendelea kutoa mchango mkubwa kwa Jamii zao. Licha ya umaskini wa kipato, bado
ni kundi linalotoa msaada mkubwa kwa kutegemeza familia pamoja na kushiriki mchakato
wa kutafuta amani na upatanisho nchini mwao.
Wanawake ni waathirika wakubwa
wa vita, kinzani na migongano ya kijamii hali inayochangiwa pia na kukomaa kwa mfumo
dume unaoendelea kuwanyanyasa wanawake na wasichana wengi Barani Afrika. Ni waathirika
wakubwa wa umaskini wa hali na kipato, rushwa na ufisadi bila kusahau utawala mbovu.
Pamoja na changamoto zote hizi, wanawake wanajikuta wakiwa na dhamana ya kuzihudumia
familia zao hasa vijijini. Umefika wakati kwa wanawake Barani Afrika kuwezeshwa kwa
njia ya elimu makini, uwezo wa kiuchumi pamoja na kumilikishwa ardhi na mali. Wanawake
vijijini na hata katika baadhi ya miji wanalazimika kutembea umbali mrefu kutafuta
maji na wakati mwingine uhaba wa nishati ya umeme wa uhakika inakuwa ni kero kubwa.
Ili kukabiliana na mwelekeo tenge wa maisha, mahali ambapo wanawake wanadhulumiwa
na kunyanyaswa, Shirika la Masista wa Upendo wa Yesu na Maria, katika kipindi cha
miaka kumi, wamekuwa mstari wa mbele kuwajengea wanawake wa Kananga uwezo wa kielimu
na kiuchumi ili waweze kuzitegemeza familia zao.
Shirika hili limekuwa likitoa
elimu kwa wasichana na wanawake ili kuboresha hali ya maisha yao kwa sasa na kwa siku
za usoni. Inasikitisha kuona na kusikia kwamba, hata katika ulimwengu mamboleo kuna
wasichana wanaolazimishwa kuolewa wakiwa na umri mdogo kabisa, yaani kati ya miaka
13 na 14, kutokana na sababu za kiuchumi na kisiasa, matokeo yake hali ya maisha inazidi
kuwa ngumu.
Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki Hispania, Manos Unidas limeendelea
kuunga mkono jitihada za Makanisa mahalia katika kuwajengea uwezo wanawake ili kupambana
na mazingira na hali yao ya maisha kwa kuwapatia ujuzi na maarifa. Lengo ni kuhakikisha
kwamba, wanawake wanaheshimiwa na kuthaminiwa hata katika mfumo dume ambao kwa sasa
umepitwa na wakati.