Vijana simameni kidete kujenga utamaduni wa haki na amani duniani
Vijana kutoka katika Baraza la Makanisa Ulimwenguni, walishiriki pia katika Maadhimisho
ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013 huko Rio de Janeiro, Brazil, kuanzia
tarehe 23 hadi tarehe 28 Julai 2013. Kauli mbiu ya Maadhimisho haya ni "basi enendeni,
mkawafanye mataifa yote kuwa ni wanafunzi."
Matukio makuu ya Maadhimisho haya
yalimshikirisha Baba Mtakatifu Francisko aliyewahimiza vijana kwenda kumtangaza Kristo
kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao. Vijana kutoka Baraza la Makanisa Ulimwenguni walishiriki
kikamilifu katika mijadala inayohusu mbinu mkakati wa ujenzi na uimarishaji wa misingi
ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kweli. Vijana walipata nafasi ya kuzungumzia
changamoto mbali mbali wanazokumbana nazo katika maisha ya ujana ambayo kwa miaka
ya hivi karibuni yamekuwa ni "nongwa".
Vijana kutoka Baraza la Makanisa Ulimwenguni
wamekazia pamoja na mambo mengine umuhimu wa vijana kujenga utamaduni wa kuheshimiana
na kuthaminiana kwa kuondokana na tabia ya ubaguzi wa rangi, hali ya kutovumiliana
kiimani na badala yake wawe ni wajenzi wakuu wa misingi ya haki na amani, kwani wao
wa hamu na ari ya kutaka kuishi, kumbe, vita ni kinyume cha hamu hii inayobubujika
kutoka katika undani wa maisha yao.
Katika Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani
kwa Mwaka 2013 vijana wamepata fursa ya kusikiliza katekesi za kina; wakashiriki katika
Maadhimisho ya Liturujia ya Neno la Mungu na Ibada ya Misa Takatifu. Ulikuwa ni muda
wa majiundo makini na fursa ya kutembelea mabanda mbali mbali ya maonesho, michezo
na majadiliano.
Vijana wamechambua changamoto katika ujenzi wa haki, utunzaji
bora wa mazingira, athari za myumbo wa uchumi kimataifa; vijana na haki msingi za
kijamii; biashara haramu ya binadamu sanjari na changamoto ya Uinjilishaji Amerika
ya Kusini. Vijana wameshiriki kikamilifu katika majiundo haya. Ni matumaini ya Baraza
la Makanisa Ulimwenguni kwamba, watajitahidi kuwa ni watangazaji hodari wa Habari
Njema ya Wokovu.