Papa achonga na waandishi wa habari kwa muda wa dakika 80 na kujibu hata maswali ya
udaku!
Baba Mtakatifu Francisko wakati akirejea kutoka kwenye Maadhimisho ya Siku ya 28 ya
Vijana Duniani kwa Mwaka 2013 huko Rio de Janeiro, amepata fursa ya kuzungumza na
waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wake kwa kuwashukuru kwa kazi kubwa walioifanya
katika kuwahabarisha walimwengu kile kilichokuwa kinatendeka huko Brazil.
Anasema,
kwake, hija hii ya kichungaji imekuwa na mafao makubwa kiroho na kimwili, kwani imekuwa
ni sherehe ya imani miongoni mwa vijana na wananchi wa Brazil, wenye moyo na ukarimu
mkubwa. Amezungumzia kuhusu usalama na kwamba, hata katika pilika pilika hizi, alipata
nafasi ya kuweza kusalimiana na kuzungumza na wananchi wa Brazil waliokuwa wanafurika
katika barabara, ingawa vikosi vya ulinzi na usalama vilikuwa na wasi wasi mkubwa,
lakini yote yamekwenda salama salimini kadiri ya mapenzi ya Mungu.
Baba Mtakatifu
anasema, anapenda kuwa karibu na watu na hili ni jambo la muhimu sana katika maisha
na utume wake. Anasema ameguswa kwa namna ya pekee kabisa na maadhimisho ya Liturujia,
Katekesi, Sanaa na za Maonesho. Ibada kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Aparecida
ni kati ya mambo ambayo yamebakiza chapa ya kudumu katika maisha yake ya kiroho. Anawashukuru
waandishi wa habari kwa kazi kubwa waliyoifanya, ingawa yeye binafsi hakupata nafasi
ya kusoma magazeti. Umati wa vijana millioni tatu ni jambo la kushangaza na la kumshukuru
Mungu. Hawa walikuwa ni wawakilishi wa vijana kutoka katika nchi 178 duniani.
Baba
Mtakatifu akijibu maswali kutoka kwa waandishi wa habari anasema, kwa sasa anaendelea
kutekeleza utashi wa Makardinali waliouonesha wakati wa mchakato wa kumchagua Khalifa
wa Mtakatifu Petro. Makardinali walipendekeza kuwa na kundi la Makardinali wanane
watakaosaidia kutoa ushauri kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro katika utekelezaji wa dhamana
na utume wake kwa Kanisa la ulimwengu katika mwelekeo wa maazimio ya Sinodi.
Kuna
mapendekezo ya kufanya mabadiliko katika Sekretarieti ya Sinodi ya Maaskofu ili iweze
kuwa ni chombo cha kudumu pamoja na kufanya mikutano ya Makardinali mara kwa mara
kwa ajili ya mafao na ustawi wa Kanisa. Mabadiliko ya Benki ya Vatican ni kati ya
mambo aliyoyapatia kipaumbele cha kwanza kutokana na unyeti wake na baada ya kikao
cha Makardinali, ilionekana kwamba, kulikuwa na haja ya kuunda Tume ambayo ingeweza
kuangalia kwa kina na mapana kuhusu masuala ya uchumi wa Vatican. Jambo la msingi
anasema Baba Mtakatifu katika masuala ya fedha na uchumi ni lazima yaongozwe na sera
ya ukweli na uwazi.
Waandishi wa habari wameulizia pia siri anayoficha kwenye
mkoba ambao umekuwa ni gumzo tangu alipoanza hija yake ya kichungaji nchini Brazil!
Baba Mtakatifu anasema, haya ni mazoea yake binafsi, daima amejibebea mkoba wake wakati
wa safari zake, hili ni jambo la kawaida, changamoto ya kuendelea kuwa ni watu wa
kawaida katika unyenyekevu.
Ndani ya Mkoba huu anasema Baba Mtakatifu anachukua
Kitabu cha Sala za Kanisa, baadhi ya vitabu anavyopenda kujisomea wakati wa mapumziko
na kwamba, anaendelea bado kuwahimiza waamini na watu wenye mapenzi mema, kusali kwa
ajili ya maisha na utume wake. Anaendelea kuishi kwenye Hostel ya Santa Martha iliyoko
mjini Vatican kwa sababu anaona umuhimu wa kuishi katika Jumuiya; ili kukutana na
kuzungumza na watu.
Kila kiongozi wa Kanisa anapaswa kuishi kadiri inavyotakiwa
na Kristo mwenyewe, bila kuonesha makuu kwani kuna watu wanaoteseka kutafuta mahitaji
yao ya kila siku, lakini bado wanajitoa sadaka kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa.
Hawa ni watu wanaoishi utakatifu katika uhalisia wa maisha ya kawaida. Hata Vatican
kama ilivyo ndani ya Kanisa kuna watakatifu na wadhambi wanaopania kujitakatifuza!
Baba
Mtakatifu anasema kuhusu suala la utoaji mimba na ndoa za watu wa jinsia moja ni mambo
ambayo Kanisa limekwishayazungumzia na kuyatolea msimamo wa kimaadili na kiutu, kumbe
haikuwa ni lazima kuyazungumzia tena, kama ambavyo hakugusia masuala ya rushwa, wizi
na ufisadi kwani yamekwishazungumziwa kwa kina na mapana na msimamo wa Kanisa unaeleweka
bayana.
Maamuzi mengine ya maisha yanapania kukuza na kudumisha majadiliano
ya kiekumene na kidini kwa ajili ya mafao na ustawi wa watu wa Mungu duniani. Askofu
anadhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Askofu anapaswa
kuandamana na waamini katika hija ya maisha yao na kamwe hapaswi kuwa ni Mfalme wa
kuabudiwa!
Kati ya matukio ambayo yako mbele yake kwa sasa ni hapo tarehe 22
Septemba 2013 atakapotembelea Kisiwa cha Cagliari. Hii itakuwa ni safari ya siku moja.
Kuna mwaliko kutoka kwa Patriaki Bartolomeo wa kwanza kuhusu Maadhimisho ya Jubilee
ya miaka 50 tangu Patriaki Athenagora alipokutana na Mtumishi wa Mungu Papa Paulo
wa sita, maadhimisho ambayo yamepangwa kufanyika mjini Yerusalemu, bado anafikiria
uwezekano wa safari hii. Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, hakupata
nafasi ya kwenda Barani Asia, hii ni changamoto kwa Papa Francisko kwa sasa. Ana mawazo
ya kutembelea Sri Lanka na Ufilippini.
Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza
wanachama wa vyama vya kitume wanaotekeleza majukumu yao kama sehemu ya mchakato wa
kujitajirisha katika maisha ya kiroho, kama wanavyofanya wanachama wa Uamsho wa Roho
Mtakatifu. Vyama hivi ni matunda ya Roho Mtakatifu na neema kwa maisha na utume wa
Kanisa. Wanachama wanapaswa kusaidiwa kutekeleza wajibu wao kadiri ya mafundisho ya
Kanisa.
Baba Mtakatifu anapongeza mchango unaoendelea kutolewa na Wanawake
Wakatoliki ndani ya Kanisa, kwani wamekuwa ni msaada mkubwa katika ukuaji wa Kanisa
sehemu mbali mbali za dunia. Ni kundi ambalo lina mchango mkubwa katika kulinda na
kudumisha utamaduni, maadili sanjari na kurithisha imani kwa vijana wa kizazi kipya.
Kanisa limekwishatoa uamuzi wa kutowapatia wanawake daraja takatifu la Upadre. Dhamana
na utume wa wanawake unapaswa kufafanuliwa vyema na taalimungu makini na wala si jambo
la hisia wala usawa katika maisha na utume wa Kanisa.
Papa Francisko amemshukuru
na kumpongeza Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, kwa maamuzi, ujasiri
na busara yake kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo. Ni mtu wa sala
na mfano wa kuigwa na wengi. Ni kiongozi anayepaswa kupendwa, kuheshimiwa, kuthaminiwa
na kusikilizwa kwa makini, kwani ndani mwake anatunza utajiri mkubwa wa maisha na
utume wa Kanisa la Kristo. Ni mtu ambaye anamsaidia Papa Francisko katika huduma kwa
Kanisa na ulimwengu katika ujumla wake.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, ndani
ya Kanisa kuna kashfa, madonda na machungu ya maisha ya kiroho yanayopaswa kuponywa
kwa njia ya: toba, msamaha na huruma ya Mama Kanisa. Hivi ndivyo Kanisa linavyochangamotishwa
kuwaangalia wanandoa waliotengana na baadaye wakaoana na watu wengine. Kuna haja ya
kuwa na mwelekeo makini wa mikakati na shughuli za kichungaji kwa wanandoa watarajiwa
bila kusahau majiundo endelevu kwa wanaoishi katika ndoa, ili waweze kutekeleza dhamana
na utume waliokabidhiwa na Mama Kanisa pamoja na Jamii katika ujumla wake.
Ndoa
na Familia ni mada zinazofanyiwa kazi kwa sasa, ili wanandoa watarajiwa waweze kuwa
na ukomavu wa kutosha katika maisha yao kwa kuelewa sheria za nchi na kanuni za Kanisa.
Baba Mtakatifu anasema yeye anajisikia kuwa ni Myesuiti kutoka katika undani
wa maisha na majiundo yake na kwamba, anatarajia kushiriki kikamilifu katika Maadhimisho
ya Siku kuu ya Mtakatifu Inyasi wa Loyola, inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka
ifikapo tarehe 31 Julai. Anasema, kama Khalifa wa Mtakatifu Petro amefurahia kukutana
na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, amesikitishwa na hali ngumu ya
maisha wanayokabiliana nayo wahamiaji na wakimbizi wanaotafuta hifadhi kwenye Kisiwa
cha Lampedusa, Kusini mwa Italia. Ameguswa kwa namna ya pekee alipokutana na watoto
wanaosoma kwenye shule za Wayesuit na alipokutana na umati wa Waseminari na Wanovisi
katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani.
Anasema, anaendelea kupata ushirikiano
mkubwa kutoka kwa viongozi pamoja na wafanyakazi wa Vatican, jambo ambalo anamshukuru
Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, alimwelezea kwa
ufupi yale yaliyojiri kwenye nyaraka za "Vaticanleak". kwa hakika ni mtu mwenye uwezo
na uelewa mkubwa!
Baba Mtakatifu Francisko anasema, moyoni mwake anasubiri
kwa furaha kuwatangaza Mwenyeheri Yohane wa ishirini na tatu na Yohane Paulo wa pili
kuwa watakatifu, viongozi wa Kanisa walioacha chapa ya kudumu katika maisha na utume
wa Kanisa. Ni watu waliojikita katika maisha ya sala, wakatoa kipaumbele cha pekee
kwa vijana waliokuwa wanaoishi katika mazingira hatarishi, ili kuwapatia matumaini
ya maisha bora zaidi. Mwenyeheri Yohane wa ishirini na tatu aliasisi Maadhimisho ya
Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, unaoadhimisha Jubilee ya miaka hamsini katika Mwaka
wa Imani, matendo makuu ya Mungu.
Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili ni mmissionari
mahiri ndani ya Kanisa, aliyethubutu kupeleka ujumbe wa Habari Njema hadi miisho ya
dunia; aliyewatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu. Baba Mtakatifu Francisko
kwa mara ya kwanza anasema, alitamani kumtangaza Yohane Paulo wa Pili kuwa Mtakatifu
hapo tarehe 8 Desemba 2013, lakini inaonekana itakuwa ni vigumu kwa waamini na watu
wa kawaida kutokana na theluji kuanza kuanguka.
Tarehe nyingine elekezi pengine
itakuwa ni wakati wa Maadhimisho ya Siku kuu ya Kristo Mfalme, tarehe 24 Novemba 2013
wakati wa Kufunga Mwaka wa Imani, lakini haitawezekana. Tarehe nyingine ni katika
Maadhimisho ya Jumapili ya huruma ya Mungu, zote hizi ni tarehe elekezi lakini bado
Kanisa linaendelea kuangalia tarehe muafaka.
kumbe, anasema Baba Mtakatifu
kwamba, tarehe 8 Desemba, 2013, Mwenyeheri Yohane Paulo wa pili, HATAWEZA KUTANGAZWA
KUWA MTAKATIFU. Wote wawili wanatarajiwa kutangazwa siku moja kuwa ni watakatifu kwani
hawa ni miamba wa imani wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.
Baba Mtakatifu
Francisko akizungumzia kuhusu shutuma mbali mbali kwa baadhi ya viongozi wa Kanisa
anasema kwamba, wale walioshutumiwa, wamefanyiwa uchunguzi wa kina na hakuna ukweli
wowote. Kuhusu mashoga anasema, si kazi yake kumhukumu mtu kutokana na hisia na jambo
la msingi ni mtu mwenyewe kutubu na kumwongokea Mungu na daima ataweza kuonja huruma
na upendo wa Mungu katika maisha yake.
Mashoga wasitengewe, wasaidie kujisikia
kuwa ni sehemu ya Jamii. Jambo linalosikitisha ni kuona kwamba, kuna watu wanataka
kutumia hisia hizi kwa ajili ya kujijenga kisiasa.
Imehaririwa na Padre Richard
Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.