Basi enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi ni ujumbe wa Yesu kwa kila mfuasi
wake na kwamba, limekuwa ni jambo la kupendeza kuona umati mkubwa wa vijana wakishiriki
katika Maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013, changamoto ya kuhakikisha
kwamba, vijana walioshiriki Maadhimisho haya wanawashirikisha na kuwaonjesha wengine
uzoefu na mang'amuzi waliyokutana nayo mjini Rio de Janeiro, Brazil.
Ni sehemu
ya mahubiri ya Baba Mtakatifu Francisko katika Ibada ya Misa Takatifu kufunga Maadhimisho
ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013. Baba Mtakatifu anawataka vijana kwenda,
bila woga kuhudumia. Haya ni maneno ambayo yamejenga msingi wa mahubiri ya Baba Mtakatifu
kwa umati wa vijana, Jumapili tarehe 28 Julai 2013.
Anasema, katika Maadhimisho
ya Siku ya Vijana wamebahatika kufanya mang'amuzi ya pamoja ya kukutana na Yesu, mwaliko
kwa sasa ni kuhakikisha kwamba, uzoefu na mang'amuzi haya wanawashirikisha wengine
bila ya kujibakiza na kamwe wasiwe wachoyo kwa kuwamegea wale walio karibu nao tu!
Vinginevyo ni sawa na kuzimisha moto wa Injili ambao tayari umekwisha washwa mioyoni
mwao.
Huu ni mwaliko wa kushirikisha mang'amuzi ya imani, kushuhudia imani
na kutangaza Injili ya Kristo kama dhamana na utume ambao Kristo amelikabidhi Kanisa
lake. Ni dhamana inayotekelezwa na watu makini, walio huru; watu wanaojisikia kuwa
kweli ni marafiki na ndugu zake Yesu. Yesu anawatuma na anaendelea kuwasindikiza katika
utekelezaji wa dhamana ya utume wa upendo.
Hapa kila mtu anashirikishwa, kwani
Injili ya Kristo ni kwa ajili ya wote na wala si kwa kikundi cha wateule wachache,
Injili inapaswa kuwafikia hata wale walioko pembezoni mwa Jamii, wale wanaoonekana
kutojali wala kuguswa na Injili.
Baba Mtakatifu Francisko anapenda kutoa changamoto
hii kwa vijana wanaotoka Amerika ya Kusini, wanaoendelea kujitoa kimasomasko kwa ajili
ya shughuli za Uinjilishaji huko Amerika ya Kusini, kumkumbuka na kumwomba Mwenyeheri
Josè de Achieta, mtume wa Brazil, aliyejitosa kutangaza Injili akiwa na umri wa miaka
18. Hii inaonesha kwamba, kijana ni chombo makini cha Uinjilishaji kwa kijana mwenzake.
Baba Mtakatifu anawataka vijana kuondokana na woga usiokuwa na msingi wowote
kwani wanapotumwa kutangaza Injili ya Kristo, anawaongoza na kuwalinda, amewaahidi
kwamba atakuwa nao siku zote hadi ukamilifu wa dahari. Yesu anawatuma kama Jumuiya
na wala si kama mtu mmoja mmoja. Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikishia vijana uwepo
wa Kanisa zima pamoja na ushirika wa watakatifu katika utume huu na kamwe wasijisikie
wapweke!
Baba Mtakatifu mwishoni mwa mahubiri yake anawataka vijana kuhakikisha
kwamba, maisha yao yanafanana na yale ya Kristo katika: fikira, mawazo na matendo.
Maisha ya Yesu ni tunu ya kuwagawia wengine, ni maisha yanayojikita katika huduma.
Ili kutangaza Injili, Mtakatifu Paulo alijifanya kuwa ni mtumwa wa wote. Uinjilishaji
ni ushuhuda wa upendo wa Mungu, unaovuka mipaka ya ubinafsi na umimi, tayari kujitoa
bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa jirani kama alivyofanya Kristo, alipowaosha
miguu wanafunzi wake.