2013-07-29 14:47:30

Papa Francisko atua mjini Roma!


Baba Mtakatifu Francisko amewasili mjini Roma tarehe 29 Julai 2013, Majira ya mchana na kupokelewa na viongozi wa Kanisa na Serikali ya Italia, kwenye Uwanja wa Ndege wa Ciampino, huku akiwa na begi lake mkononi. Kabla ya kushuka kwenye ndege, Baba Mtakatifu aliweza kuzungumza na wafanyakazi wa ndege na kuwashukuru kwa ukarimu na huduma waliyomwonesha.

Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii anasema kwamba, amekwishawasili mjini Vatican na anapenda kuwahakikishia kwamba, furaha iliyojaa moyoni mwake ni kubwa zaidi kuliko hata uchovu wa safari kutoka Rio de Janeiro.

Baba Mtakatifu alipowasili mjini Roma amekwenda moja kwa moja kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu kwa ajili ya kusali na kumshukuru Bikira Maria kwa maadhimisho na mafanikio yaliyopatikana katika Maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013. Kuna baadhi ya vijana waliokuwa kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria walipomwona Baba Mtakatifu anaingia, walikwenda kumsalimia na kumpatia zawadi ambazo amezitoa kwa Bikira Maria.

Hayo yamesemwa na Padre Federico Lombardi, msemaji mkuu wa Vatican aliyekuwa kwenye msafara wa Baba Mtakatifu nchini Brazil kwa takribani juma zima. Wachunguzi wa mambo wanasema kwa hakika Baba Mtakatifu Francisko amefunika nchini Brazil.







All the contents on this site are copyrighted ©.