2013-07-29 14:50:11

Papa atuma salam za rambi rambi kutokana na kifo cha Kardinali Tonini


Baba Mtakatifu Francisko amepokea kwa masikitiko makubwa habari za kifo cha Kardinali Ersilio Tonini, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Ravenna- Cervia. Anapenda kuwahakikishia wote wanaoomboleza msiba huu mkubwa uwepo wake kwa njia ya sala na sadaka kwa kumpoteza mchungaji mchapakazi na mkarimu, aliyejipambanua kutokana na utume wake katika medani mbali mbali za maisha na utume wa Kanisa.

Ni kiongozi aliyemtangaza Kristo kwa watu wote huku akitumia lugha nyepesi pamoja na kuonesha ushuhuda wa maisha kwa watu wa nyakati hizi. Ujumbe wa Baba Mtakatifu umeandikwa kwa niaba yake na Kardinali Tarcisio Bertone, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Askofu mkuu Lorenzo Ghizzoni wa Jimbo kuu la Ravenna. Baba Mtakatifu anawapatia baraka zake za kitume, wote wanao omboleza msiba huu.







All the contents on this site are copyrighted ©.