2013-07-29 08:46:33

Maadhimisho ya Siku ya 29 ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2016 yatafanyika Cracovia, Poland


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kama sehemu ya Maadhimisho ya kufunga Siku ya 28 ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013, amewashukuru viongozi wa Baraza la Kipapa la Walei na Kanisa Katoliki nchini Brazil kwa kufanikisha Maadhimisho haya.

Baba Mtakatifu amewaweka vijana wote chini ya ulinzi na usimamizi wa Bikira Maria, ili waweze kujifunza kuwa ni wafuasi na wamissionari hodari. Katika Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, vijana wameonja uzuri wa kumfuasa Kristo wakiwa wameandamana na Kanisa kwa kutambua kwamba, Injili ni jibu makini linalozima kiu ya utimilifu wa maisha.

Bikira Maria ni kielelezo makini cha kuwa Mfuasi na Mmissionari wa Kristo. Baada ya kupokea neema ya kuwa ni Mama wa Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, Bikira Maria aliamua kushirikisha zawadi hii kwa njia ya huduma kwa binamu yake Elizabeth aliyekuwa anahitaji msaada. Kwa njia hii, Bikira Maria alitekeleza tendo la upendo kwa njia ya huduma makini, akimbeba Mtoto Yesu tumboni mwake. Bikira Maria alitekeleza huduma hii kwa haraka na kwa njia hii, ni mfano na kielelezo kwa wafuasi wa Kristo.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika vijana kumwomba Bikira Maria ili aweze kuwasaidia kujitosa bila ya kujibakiza kwa ajili ya wote wanaohitaji msaada. Baba Mtakatifu amehitimisha tafakari ya Sala ya Malaika wa Bwana kwa kutaja kwamba, Maadhimisho ya Siku ya 29 ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2016 yatafanyika Jimbo kuu la Cracovia, Poland.







All the contents on this site are copyrighted ©.