Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa vijana katika Maadhimisho ya Siku ya Vijana
Duniani huko Rio de Janeiro, Brazil ni mzito kweli. Maana ya utakatifu si muonekano
wa nje bali ni badiliko la ndani, ni toba na wongofu wa ndani; ni upya uliofichika
katika nafsi za vijana na uthabiti wa maisha yao machanga ya Ushuhuda na ya Kikristu
katika dunia hii geu geu.
Hii itawapa moyo sana vijana ambao katika jicho
la wazee walionekana wamechafua "utakatifu" wao kwa kunywa Coca Cola, kuzama kati
I pads zao au kwenye matamasha ya muziki.
Haya ni mang’amuzi ya Padre Beno
Michael Kikudo kutoka Jimbo kuu la Dar es Salaam, anapojaribu kuwashirikisha wana
ukoo wenzake kuhusu changamoto za utakatifu wa maisha, kama ulivyofafanuliwa na Baba
Mtakatifu Francisko wakati alipokuwa anakutana na vijana nchini Brazil.
Vijana
waliona utakatifu kwao ni kama “msamiati wa Kichina au kitu kisichowezekana kuishika
wala kumwilishwa katika uhalisia wa maisha. Vijana walidhani kwamba, utakatifu ni
maisha ya kufikirika na kusadikika waliyoishi watu wa kale. Vijana waliona maisha
yao kama wasindikizaji tu wa kundi jingine dogo linalotafuta utakatifu na hao kwa
nasibu wamesalia katika nyumba za kitawa na maparokiani
Hatari ya kuacha na
kuendeleza muono wa utakatifu katika dhana ya maisha magumu, yasiyopendeza na ushahidi
mkali wa kumwaga damu tu - hatari yake ni kugandisha hamu ya kuwa watatifu katika
nyumba za watawa na maghorofa ya makasisi.
Tuombe Mungu vijana wang'amue kweli
kile ambacho Baba Mtakatifu Francisko alikusudia kusema kwao. Yaani, waone utakatifu
katika jicho na mwanga mpya kama Bartimayo kipofu wa Yeriko (Marko 10:51) - "Mwalimu
naomba nipate kuona tena.."