2013-07-29 09:21:44

Inapendeza kutoa kuliko kupokea!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 28 Julai 2013 alikutana na vijana waliokuwa wanajitolea kutoa huduma, akawashukuru kwa moyo wa ukarimu na uungwana waliouonesha kwa vijana wenzao wakati wa Maadhimisho ya Siku ya 28 ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2013 huko Rio de Janeiro, Brazil. Baba Mtakatifu anasema, ni kheri kutoa kuliko kupokea kama yanavyosema Maandiko Matakatifu.

Katika Maadhimisho ya Siku ya Vijana, wameshiriki kwa njia ya huduma, kama alivyofanya Yohane Mbatizaji kabla Yesu kuanza maisha ya hadhara, akamwandalia mapito. Kwa upande wa vijana waliokuwa wanajitolea, wamekuwa ni chombo cha maandalizi kwa ajili ya vijana kuweza kukutana na Yesu.

Baba Mtakatifu anawakumbusha kwamba, Mwenyezi Mungu ana mpango na kila mmoja wao, jambo la msingi ni kugundua mpango wa Mungu katika hija ya maisha yao na hatimaye, kuufanyia kazi. Mwenyezi Mungu anawaalika wote kuwa ni watakatifu na kila mmoja anaweza kuufikia utakatifu wa maisha kwa njia tofauti. Baadhi ya waamini wanaalikwa kuwa watakatifu kwa njia ya Sakramenti ya Ndoa Takatifu, ili kujenga familia na kwamba, ndoa ni zawadi kubwa ambayo Mwenyezi Mungu anawakarimia waja wake ili kushiriki katika kazi ya Uumbaji inayowawajibisha.

Baba Mtakatifu anaonya kwamba, kuna baadhi ya watu wanadhani kwamba, ndoa ni mambo yaliyopitwa na wakati, lakini kwa waamini hii ni dhamana endelevu, changamoto ya kuwa na maamuzi thabiti yanayowawajibisha katika Kanisa na Jamii inayowazunguka.

Baba Mtakatifu anasema kwa wale wanaoamua kuchagua wito wa Upadre, wanapaswa kujitosa kimasomaso bila ya kujibakiza, wakipenda na kutenda kama Yesu mchungaji mwema. Baadhi ya waamini wanaitwa pia kuwa ni watawa, ili kujitoa kwa ajili ya sala na sadaka ya maisha yao kwa ajili ya mafao ya wengi, katika medani mbali mbali za maisha, lakini zaidi kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.

Baba Mtakatifu amewakumbusha kwamba, hata yeye alisikia wito wa kuwa ni Mtawa na Padre alipokuwa na umri wa miaka 17, changamoto kwa vijana kutokuwa na woga wa kusikiliza na kutekeleza kile ambacho Mwenyezi Mungu anataka kutoka kwao. Ni vyema kukubali mpango wa Mungu katika maisha yao, kwani Mungu ni chemchemi ya furaha ya kweli.

Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha hotuba yake kwa vijana waliokuwa wanajitolea kwa kuwataka kujiuliza swali la msingi, Je, Mwenyezi Mungu anataka nini katika maisha yao! Je, ni njia ipi wanayopaswa kuifuata ili kufikia lengo la maisha na wito wao!







All the contents on this site are copyrighted ©.